Shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika (CAF ), kawaida hutoa nafasi nne (4) za ushiriki wa klabu ambazo nchi yake ipo miongoni 12 bora kwa viwango barani Afrika.
Ubora wa kila nchi hupimwa kwa mafanikio ya klabu zake kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Tanzania ni ya 12 ikiwa na pointi 18 ilizovuna kutokana na mafanikio ya Yanga na Simba katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.
Yanga iliingia mara mbili (2) hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016 na 2018. Hatua kama hiyo huipatia nchi husika pointi 2.5.
Hivyo pointi 2.5 za 2016 na 2018 kutoka kwa Yanga zikaipatia Tanzania jumla ya pointi 5 na Simba ikaingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu wa mwaka 2018/19.
Wakati hatua kama hiyo ya Simba huipatia nchi husika pointi 15. Hivyo basi Tanzania ilistahili iwe na pointi 20 jumla, yaani 5 za Yanga na 15 za Simba.
Swali la kujiuliza iweje hazipo ?
Kiutaratibu, CAF hupima viwango vyao kwa mafanikio ya ndani ya kipindi cha miaka mitano ( 5 ) iliyopita. Na kila mwaka mmoja unapoongezeka thamani ya pointi za mwaka wa nyuma zaidi hupungua.
Kwa mafanikio ya Simba, 2018/19, hesabu zake za miaka mitano ( 5 ) zilianzia 2015. Hivyo, pointi 5 za Yanga zilipungua thamani mwaka 2019, na kubaki 3 na zilipojumlishwa na zile 15 Simba za 2018/19, ndiyo zikawa 18.
Baada ya Simba, Azam, KMC kutolewa mapema katika mashindano hayo ya Afrika hatma ya Tanzania ipoje ?
Kutokana na utaratibu huo, msimu ujao wa mashindano ya Afrika, 2019/21, Tanzania itabaki na pointi 17 kwa sababu zile 3 za Yanga, zitabaki.
Kwa maana hiyo, hatari ya Tanzania kupoteza nafasi 4 za ushiriki ni kubwa mno, endapo Yanga watashindwa kufika hatua ya Makundi kombe la Shirikisho.
Wawakilishi pekee katika michuano ya Kimataifa, Yanga kama watatinga hatua ya makundi itapatia Tanzania pointi 2.5 ambazo sasa zitaongezwa na zile 17 zitakazobaki na kuwa 19.5.
Na kama Yanga itafanya vizuri zaidi mbali tu ya kutinga hatua ya makundi na badala yake kushika nafasi ya 3 katika ‘group’ lake, basi itapata pointi 5, na Tanzania itakuwa na pointi 22.
Na kama ikifika robo fainali, itaipatia Tanzania pointi 10, zikiongezwa na 17, tutakuwa na pointi 27. Hapo nafasi yetu itakuwa salama salmini.