Miraji Athuman (26) ni mshambuliaji mpya wa Simba ambaye anaonesha matumaini makubwa kwa mashabiki wa Simba ya kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi ndani ya kikosi hicho kutokana na staili yake ya uchezaji.
Juhudi yake uwanjani pindi anapopewa nafasi, umakini wake wa kufuata maelekezo ya kocha pamoja na maneno yake kwenye mahojianao tofauti tofauti, vinaonesha ni namna gani ambavyo amekomaa hivi sasa kucheza katika kikosi hicho.
Mpaka hivi sasa amefunga jumla ya mabao matatu, mawili kati ya hayo amefunga akitokea benchi na bao moja amefunga jana baada ya kuanzishwa katika kikosi cha Simba kilichoshinda mabao 2-0 dhidi ya Biashara United.
Mwenyewe anasema kuwa siri kubwa inayomsaidia kupata bao kila anapopata nafasi ni namna anavyokuwa makini kuwasoma wapinzani pindi anapokuwa benchi, hivyo huwa anatumia makosa hayo kuwaadhibu anapoingia.
"Kitu kikubwa ninchokifanya kabla sijaingia uwanjani ni kuwasoma wapinzani na nikiingia, kikubwa nina furaha kwa sababu malengo yangu ni kuweza kucheza na kufunga magoli kila mechi", amesema Miraji, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana dhidi ya Biashara United.
Ikumbukwe kuwa Miraji Athuman amepitia vilabu kadhaa kabla ya kurejea tena Simba ambako ndiko kipaji chake kimeanzia na kuaminiwa, miongoni mwa vilabu hivyo ni Toto Africans (2015-2016), Mwadui FC (2016-2018), Lipuli FC (2018-2019).
No comments:
Post a Comment