ALIYEKUWA mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi ambaye hivi karibuni alitangaza kuachana na klabu hiyo, kuna uwezekano mkubwa akarejea tena kikosini hapo kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni Okwi aligoma kuongeza mkataba wa kuitumikia Simba baada ya kushindwana katika suala zima na fedha na hivi karibuni ikaripotiwa kuwa amejiunga na timu ya Fujairah FC ya Falme za Kiarabu (UAE).
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatano limezipata zimedai kuwa dili hilo la Okwi la kujiunga na Fujairah limeingia doa, hivyo yupo katika mchakato wa kurudi Simba. Akizungumza na Championi Jumatano, mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema kuwa uongozi pia umeonekana kukubaliana na suala hilo.
“Baada ya Okwi kugoma uongozi ulikuwa na mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Nkana ya Zambia, Walter Bwalya lakini mpango huo uliingia doa baada ya timu ya El Gouna FC ya nchini Misri kutuzidi kete kwa kutoa dau kubwa mara mbili zaidi yetu, wakamsajili.
“Baada ya hapo nguvu zetu tukazielekeza kwa mshambuliaji wa Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini, Justin Shonga, lakini kabla hatujakaa sawa Al Ahly ya Misri pia wakaingilia dili hilo na kutangaza kumsajili kwa fedha nyingi zaidi ya zile za kwetu.
“Kutokana na hali hiyo hatukuwa na jinsi ikibadi turudi kwa Okwi ambaye kwa sasa mazungumzo yanaenda vizuri kabisa na tunataka kumsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja, kwa hiyo kama ulisikia kuna sapraizi inakuja basi anaweza kuwa Okwi,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Hata hivyo, alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori kuzungumzia hilo hakupatikana lakini taarifa ambazo gazeti hili lilizipata zimedai kuwa hawataki kulizungumzia hilo kwa sasa.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua jengo la tatu la abiria kwenye kiwanja cha ndege cha Mwalimu Nyerere ili kuona maandilizi ya mapokezi kwa wajumbe wa mkutano wa SADC.
Akizungumza na watendaji wa Serikali pamoja na Kamati ya maandalizi uwanjani hapo leo jioni (Jumatano, Julai 31, 2019), Waziri Mkuu amesema maandalizi ni mazuri isipokuwa kwa kasoro chache zilizobakia.
“Nimepita VIP hakuna shida. Pale terminal 2, sehemu ya Uhamiaji iko vizuri, uchunguzi wa afya nayo iko vizuri, lakini vyoo inabidi vibadilishwe haraka sana. Vile vyoo pale nje vimechoka, vibadilishwe mara moja, siyo tu kwa ajili ya ugeni, bali ni kwa faida yetu pia,” amesema huku akimwagiza meneja wa uwanja huo, Bw. Paul Lugasha aharakishe zoezi hilo.
Katika jengo la tatu la abiria kwenye uwanja huo, Waziri Mkuu amekagua eneo ambalo viongozi wakuu wa nchi watashukia, watakagua gwaride la heshima na kuangalia vikundi vya ngoma. Pia amekagua vyumba ambavyo watapumzikia kabla ya kuelekea mjini.
Amesisitiza kuwa usafi wa barabarani bado hauridhishi sababu kuna mawe, udongo na michanga kwenye barabara kuu ya kutoka uwanja wa ndege hadi mjini. “Tulikubaliana kuwa zile bustani ziboreshwe, vyuma vya barabarani vitengenezwe lakini hata leo nimepita kwenye fly-over, bado kuna mawe na michanga, hata sijui vinatokea wapi,” alisema.
Amewataka wahusika waweke banners za kutosha za aina mbalimbali na picha za wanyama kutani, uwanjani hapo ili kuonesha kwamba kuna mkutano mkubwa unafanyika hapa nchini.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka Watanzania watumie fursa ya uwepo wa mkutano huo mkubwa kuendesha biashara zao na ujasiriamali.
“Ziko fursa nyingi za uwepo wa mkutano huu. Kila mmoja atumie nafasi hii kuweza kuongeza na kuboresha kazi yake inayomletea uchumi,” amesema.
(mwisho) IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU, JUMATANO, JULAI 31, 2019.
Uongozi wa klabu ya Yanga umekamilisha usajili wa mshambuliaji David Molinga kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea klabu ya AC Lega ya DR Congo
Molinga alitua usiku wa kuamkia leo kukamilisha usajili wake kabla ya dirisha la usajili kufungwa saa 5:59 usiku wa leo
Molinga anachukua nafasi ya mlinda lango Klaus Kindoki ambaye inaelezwa amefikia makubaliano na uongozi wa timu hiyo kupelekwa kwa mkopo kunako klabu yake ya zamani Fc Lupopo ya DR Congo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedeyoka amesema jeshi hilo halijavunja kongamano lililoandaliwa na kamati ya maridhiano Zanzibar na kuhudhuriwa na Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT - Wazalendo, Maalim Seif Sharrif Hamadi pamoja na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe.
Sedeyoka amesema kilichotokea ni kwamba askari wa doria walipita eneo hilo na kubaini mkusanyiko wa watu na kutaka warejee kwenye shughuli zao za kila siku inavyokuwa, na kwamba hawakumuondoa Maalim Seif kama ilivyokuwa ikiripotiwa.
Kwa upande wa Zitto Kabwe akizungumza mara baada ya kongamano hilo kuzuiliwa amesema, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Malindi alifika eneo la Kongamano na kutoa amri mbili ikiwemo ya kutaka kumkamata Maalim Seif ama kusimamisha kongamano.
"Hamna mtu ambaye anaweza kuthubutu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumchukua maalim kwa nguvu, tuna wanasheria kuna taratibu za namna za kumhitaji kiongozi mwenye hadhi ya Maalim hawezi tu kuja Mkuu wa Kituo cha Polisi Malindi na kutoa amri. Maalim ni mtu ambaye amekuwa sehemu ya viongozi katika nchi hii, amekuwa Waziri Kiongozi na Makamu wa kwanza wa Rais'', amesema Zitto.
Aidha Zitto amesema kuwa huenda polisi walikuwa na lengo la kuvuruga mkutano na kuzuia Wazanzibar kujadiliana juu ya neema zilizokuwepo wakati wa maridhiano.
Mwanasheria Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Tundu Lissu amesema amehitimisha matumizi ya dawa alizoanza kuzitumia tangu Septemba 7 mwaka 2017. Lissu alianza kutumia dawa hizo Septemba 7 mwaka 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma ambapo tangu wakati huo amekuwa akipatiwa matibabu nje ya nchi.
Katika salamu kwa marafiki zake alizozitoa leo Jumatano Julai 31, 2019, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Lissu ameandika;
Hello Marafiki wa Mimi,
Habari za masiku mengi. Sijawasemesha kwa kitambo kidogo. Nisameheni bure, nafikiri mnafahamu jinsi ambavyo mambo yamekuwa mengi. Nina mambo mawili, nayo ni mema tu. .
La kwanza linahusu hali yangu ya afya. Leo tarehe 31 Julai, 2019, ni siku ya kwanza tangu niliposhambuliwa Septemba 7, 2017, situmii dawa ya aina yoyote. .
Kwa maelekezo ya madaktari wangu, jana ilikuwa siku ya mwisho ya mimi kutumia madawa ambayo nimeyatumia tangu siku niliposhambuliwa. .
Na jana hiyo hiyo nilitimiza mwezi mzima tangu niache kutumia magongo. Ijapokuwa bado nachechemea kwa sababu ya goti kutokukunja sawa sawa, sasa ninatembea bila msaada wa magongo. .
Safari yangu, na yetu, ndefu ya matibabu itakamilika Agosti 20 nitakapokutana na timu ya madaktari wangu kwa ajili ya vipimo vya mwisho na ushauri. .
Baada ya hapo itakuwa ni maandalizi ya kurudi makwetu. Hakutakuwa na sababu tena ya kitabibu ya mimi kuendelea kukaa Ulaya. .
Kwa vile tumekuwa pamoja kwenye safari hii ndefu, hatuna budi kupongezana na kumshukuru Mungu kwa hatua hii nzuri nilikofikia. Mimi na familia yangu hatutachoka kuwashukuru sana kwa kuwa pamoja nasi katika kipindi chote hiki kigumu. Mungu awabariki sana. .
La pili linahusu ubunge wangu. Tangu Spika Ndugai anivue ubunge, sijasema maneno mengi sana, zaidi ya kusema kwamba tutaenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo. .
Kesi za ubunge, kama zilivyo kesi zote za uchaguzi wa kisiasa, ni kesi za kisiasa. Ni mwendelezo wa mapambano ya kisiasa katika uwanja tofauti. .
Kwa sababu hiyo, ni kesi nyeti na za kipekee sana. Zinahitaji umakini mkubwa katika kuziandaa na kuziendesha. Nina uzoefu mkubwa nazo, kwa sababu nimezifanya sana tangu 2005.
Sasa ninaweza kuwafahamisha kwamba mimi na timu ya mawakili wangu tuko tayari kuingia Mahakama Kuu ya Tanzania. Tutafanya hivyo muda wowote kuanzia leo. Maandalizi yote yanayohitajika yamekamilika.
Tunataka kuiomba Mahakama Kuu itoe jibu la swali alilouliza Spika Ndugai na walio nyuma yake: je, Spika wa Bunge la Tanzania ana uwezo kikatiba na kisheria, wa kufuta ubunge wa mbunge yeyote yule, kwa sababu yoyote ile, bila kumuuliza mbunge husika jambo lolote kuhusu sababu za kumfuta ubunge huo??? .
Nitawajulisheni mara moja kesi hii itakaposajiliwa rasmi. Kama itawapendeza, nitawaomba mtakaopata nafasi kuhudhuria mahakamani, kwa niaba yangu, wakati wote kesi hiyo itakapokuwa inaendelea. .
Nilitaka kuwashirikisheni haya kwa leo. Nawashukuruni sana na Mungu awabariki sana
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof.Joyce Ndalichako,amegiza kuondolewa katika nafasi zao Afisa Mdhibiti Ubora wa Elimu Kanda ya Magharibi, Khalid Nuru, Afisa Mdhibiti Ubora Msaidizi Paul Bigashina Afisa Mdhibiti Ubora wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, kwa kukaidi maagizo ya mamlaka.
July 18 mwaka huu Prof. Ndalichako,alitembelea na kukagua ujenzi wa ofisi za udhibiti ubora wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo aliagiza kubomolewa na kurekebishwa baada ya kutoridhishwa na vipimo vya saruji vilivyotumika katika hatua ya sakafu ya ujenzi huo.
Hata hivyo katika ziara yake ya ghafla aliyoifanya leo amebaini maelekezo yake kutotekelezwa na kumuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, kuwaondoa wadhibiti ubora hao na kuwapangia kazi nyingine.
Umoja wa Ulaya (EU) umesema umeshtushwa na kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mhandisi Leopold Lwajabe, ambaye mwili wake ulikutwa ukining'inia juu ya mwembe katika kijiji cha Mgoza Wilayani Mkuranga siku ya Julai 26, 2019.
''Tumesikitishwa na taarifa za kifo cha Lwajabe, ni mwenzetu, ni rafiki yetu mzuri, kifo chake kimetustua sana'', imesema taarifa ya EU.
Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa utendaji na kujitoa kwake katika kazi kwa miaka kadhaa ni wa kuthaminiwa na wako bega kwa bega katika kutoa ushirikiano wao kwa ndugu na Wizara ya Fedha katika kipindi hiki kigumu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya DSM leo Julai 31, imeeleza kuwa Lwajabe alijinyonga huku akiacha ujumbe wa wosia ofisini juu ya meza yake akitoa mgawanyo wa mali kwa ndugu zake ikiwemo mashamba, nyumba, gari, ng'ombe na viwanja.
Wosia mwingine aliouacha ni wa kuchinjiwa ng'ombe takribani wanne wakati wa maombolezo ya msiba wake.
Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ameamuru waratibu 24 TASAF ngazi ya Wilaya wakamatwe kwa kuruhusu marehemu hewa walipwe fedha za TASAF na kuisababishia hasara ya zaidi ya Milioni 300 kwa Serikali kwa kuruhusu Kaya hewa 1000 kulipwa fedha hizo.
Jeshi la Polisi Zanzibar limezuia kongamano lililoandaliwa na kamati ya maridhiano Zanzibar na kumuondoa ukumbini, Mshauri mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif.
Tukio hilo limetokea leo mchana Jumatano Julai 31, 2019 kabla ya kuanza kongamano hilo katika ukumbi wa Bitulyamin Malindi mjini Unguja, Zanzibar.
Hata hivyo, bado haijaelezwa chanzo cha kuzuiliwa kwa kongamano hilo. Ingawaje naibu katibu wa kamati ya habari Zanzibar wa ACT-Wazalendo, Seif Hamad, amedai kuwa walifuata masharti yote ya kuomba vibali vya kongamano hilo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ametolea ufafanuzi kifo cha mtumishi wa Wizara ya fedha, Leopard Lwajabe (56), ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umening’inia kwenye mti wa muembe katika kijiji cha Mgoza wilayani Mkuranga.
Mambosasa amesema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa eneo la tukio hakukuwa na viashiria vyovyote vya kujitetea wakati wa tukio na kwamba mwili wa marehemu hakukuwa na jeraha lolote isipokuwa shingoni kulikokuwa kumefungwa kamba iliyotumika kujingonga.
Ametoa ufafanuzi huo leo Jumatano Julai 31, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema mnamo Julai 26 mwaka huu Polisi Kanda Maalum ya Rufiji walipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Mgoza, Mohamed Said (68), kwamba kumeonekana mwili wa mwanaume ukiwa unang’inia kwenye mti wa muembe na polisi walipofika waliukuta mwili huo ukionesha mhusika amenyinyonga.
“Julai 29, mwaka huu walipatikana ndugu wawili wa marehemu ambao ni Chumila Mwalimu mkazi wa Manyara na Jonathan Herman ambaye ni mfanyakazi mwenzake na marehemu ambao walifanikiwa kuutambua mwili na kueleza kuwa marehemu alitoka nyumbani kwake kwenda ofisini akiwa na dereva wake na baadae alimtuma dereva akamchukulie simu nyumbani kwake Kinyerezi na baada ya hapo marehemu alitoweka ofisini na kwenda kusikojulikana hadi alipogundulika amejinyonga,” amesema.
“Mnamo Julai 29, wafanyakazi waligundua kuwa marehemu aliacha notebook mezani kwake iliyokuwa na mgawanyo wa mali zake ambapo aliruhusu kati ya ng’ombe anaofuga wanne watumike katika msiba wake na pia simu aliyomtuma dereva iligundulika kuwa imeshafutwa kumbukumbu zote,” amesema.
Aidha amesema mwili wa marehemu ulihamishiwa hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi na ilibainika kifo hake kilisababishwa kwa kujinyonga ambapo chanzo hakijafahamika mpaka sasa na upelelezi uaendelea.
“Mtu aliyeuawa mahali halafu akaeda kufungwa kuna vitu vinavyokosekana kwa mfano mtu anayejinyonga lazima aachie haja ndogo na kubwa kwababu ya nguvu ya roho kutoka na hivyo vyote vimekutwa aneo la tukio,” amesema Mambosasa.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya jumla ya TZS 15.9 trilioni kati ya lengo la TZS 18 trilion kwa mwaka wa Fedha 2018/19 kuanzia tarehe 1 Julai 2018 hadi 30 Juni 2019. Aidha katika robo ya nne ya mwaka huo wa fedha yaani, mwezi Machi hadi Juni 2019, TRA ilikusanya TZS 1.1 trilioni, TZS 1.2 trilioni, na TZS 1.5 trilioni kwa mwezi Aprili, Mei, na Juni, mtawalia. Kwa namna ya kipekee kabisa, TRA inawashukuru walipakodi na wananchi wote kwa ujumla kwa ushirikiano.
Ikumbukwe kwamba, katika mwaka huo wa fedha, Serikali ilianzisha Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) ambao utekelezaji wake umefanyika kwa awamu mbili (2). Awamu ya kwanza, ilihusisha bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia na aina zote za vileo. Awamu hii ya kwanza iliyoanza kutekelezwa tarehe 15 Januari 2019 imeendelea vizuri na maandalizi ya awamu ya pili ya utekelezaji wa ETS inayojumuisha bidhaa za vinywaji baridi, maji, juisi, na CD/DVDs yamekamilika. Hivo mfumo huu wa ETS kwa awamu hii ya pili, unatarajiwa kuanza kazi rasmi tarehe 1 Agosti, 2019.
Lengo kuu la kubandika stempu hizi za kielektroniki ni kuongeza usimamizi na ufanisi wa ukusanyaji wa Ushuru wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kupata taarifa sahihi za uzalishaji viwandani ili kukusanya mapato stahiki.
Ni matumaini ya TRA kuwa, wazalishaji, waingizaji, wasambazaji, wauzaji wote wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa pamoja, na umma kwa ujumla wataendelea kutoa ushirikiano kwa TRA ili kufanikisha utekelezaji wa mfumo huu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu” Richard M. Kayombo KAIMU MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI
Mkuu wa wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera Kanali Denice Mwila amewataka wananchi wilayani missenyi kuacha tabia za kuwapokea na kuwahifadhi wahamiaji haramu kutoka nchi jirani jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Kanali MWILA ametoa kauli hiyo na kusema kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikipelekea wahamiaji haramu kuongezeka wilayani missenyi mkoani hapa hivyo kupelekea watanzania kukosa ardhi ya kulima na kufanya shughuli za ufugaji.
Kutokana na hali hiyo,kanali MWILA amesema kuwa watanzania katika maeneo ya mipakani hususani kata za Mtukula,Kakunyu na Minziro wanatakiwa kuhakikisha wanaepuka kupokea rushwa kutoka kwa wahamiaji ili wawape hifadhi.
Amesema kuwa serikali wilayani humo haitawafumbia macho wananchi watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Klabu ya soka ya Yanga imewapiku mahasimu wao wa jadi Simba katika kutambulisha wimbo rasmi wa klabu kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Yanga imetambulisha wimbo wake rasmi utakaotumiwa katika michuano mbalimbali kuanzia msimu huu, na kusisitiza kuwa ni wajibu wa wanachama na mashabiki kuufahamu wimbo huo.
Wimbo huo wa Yanga utaanza kutumika katika mchezo wao wa Kimataifa wa 'Wiki ya Wananchi', Agosti 4 dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya.
Mahasimu wao Simba waliahidi kutoa wimbo wao rasmi wa klabu ifikapo Agosti 3, 2019, wimbo ambao utaanza kutumika katika mchezo wao wa Kimataifa wa Simba Day, Agosti 6 dhidi ya Power Dynamo ya Zambia.
Kampuni ya UHL Dubai imeshinda Tenda ya kutengeneza jezi za klabu ya Simba kwa ajili ya msimu wa 2019/20
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori amesema kampuni hiyo ambayo inashirikiana na kampuni ya Romario, wamesaini nayo mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Tsh Milioni 600, kila mwaka ni Tsh Milioni 300
Aidha kampuni ya Romario ndio itakayohusika kwenye uuzaji wa jezi za Simba msimu huu. Thamani ya jezi watakazozitoa ni Tsh Milioni 200
Jezi zitaanza kuuzwa kuanzia kesho Alhamisi, zikipatikana kwa bei ya Tsh 30,000/-
Kwa hapa Dar es salaam, jezi zitapatikana maeneo ya Sinza, Posta na Makao Makuu ya klabu ya Simba, Kariakoo mtaa wa Msimbazi
Kwa watakaohitaji jezi zinazotumiwa na wachezaji, bei yake ni Tsh 120,000/-
Kamishna wa Uraia na Pasipoti Uhamiaji, Gerald Kihinga amesema kuwa Mwandishi wa habari, Erick Kabendera aliyedaiwa kutoweka nyumbani kwake idara ya uhamiaji wanae na wanaendelea kumhoji utata wa uraia wake.
Kamishna Kihinga amesema kuwa Uhamiaji walipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema kufuatia utata wa uraia bwana Erick Kabendera.
"Uhamiaji tulipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema kufuatia utata wa uraia wa bwana Erick Kabendera baada ya idara kupewa tarifa hizo tulianza kuzifanyia kazi hata hivyo Kabendera mwenyewe hajawahi kuhojiwa kulingana na Uraia wake kwakuwa hakufika katika ofisi ya uhamiaji pamoja na kutumiwa wito mara nyingi lakini hakuweza kufika, " amesema Kamishna Kihinga.
"Uhamiaji kushirikiana na jeshi la Polisi tuliweza kumtafuta na kumpata na mpaka tunavyoongea hivi bwana Kabendera tunae sisi uhamiaji kwaajili ya kumhoji kuhusu utata wa uraia wake.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kigwangalla, ameipa siku saba Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuhakikisha wanapeleka mapendekezo ya namna gani watawahakikishia wawekezaji malighafi.
Katika mapendekezo hayo, amewataka kila mwaka walau kwa kipindi kisichopungua miaka mitano waweze kukopesheka kwa urahisi.
Dk. Kigwangalla amesema hayo, alipokuwa akizungumza katika mkutano wake na wadau wa Sekta ya Misitu uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambapo amesikiliza changamoto zinazowakabili na kuahidi kuzifanyia kazi.
“Kuhusu suala la mikataba ya kuwazia wadau wetu vitalu, TFS ninawapa siku saba mniletee mapendekezo ya kina ni kwa namna gani tunaweza kuwahakikishia wadau wetu ambao ni wawekezaji kwenye viwanda kwa sababu tuna uwezo wa kuwatambua sasa tunawezaje kuweka utaratibu ambao utawahakikishia malighafi kila mwaka walau kwa kipindi kisichopungua miaka mitano ili waweze kukopesheka kwa urahisi ,” amesema.
“Hili ni jambo ambalo halipaswi kushindikana hivyo mjipange mtakavyoweza lakini mtuletee wizarani mapendekezo ni kwa namna gani mtaweka uhakika kwa wadau wetu ambao ni wawekezaji kwenye sekta ya bidhaa ya misitu watapa malighafi kwa uhakika walau katika kipindi cha miaka mitano,” amesema.
Aidha amesema kuwa kwa mwaka Tanzania inaharibu misitu katika eneo la ukubwa wa hekari laki 4.5, ambapo amewapongeza wakazi wa mikoa kusini na baadhi ya mikoa ya Kaskazini na Kaskazini Magharibi kwa jitihada wanazozifanya za kupanda miti kibishara kwa kusema wanasaidia katika ikolojia ya maisha duniani,” amesema Dk. Kigwangalla.
Mashabiki wenye hasira wa Korea Kusini wanataka walipwe fidia baada ya Cristiano Ronaldo kushindwa kuingia uwanjani wakati wa mchezo wa kirafiki wa kabla ya msimu dhidi ya Juventus. Nyota huyo wa Ureno alikuwa amesaini mkataba wa kucheza dakika 45 wakati mechi dhdi ya timu hiyo ya Ligi K ya nyota wote ilipotangazwa , wanasema waandalizi, lakini alikaa kwenye benchi nje ya uwanja.
Mashabiki walijawa na ghadhabu wakati aliposhindwa kuonyesha ishara yoyote ya kuingia uwanjani, hata wakaanza kushangilia kwa kupaza sauti wakilitaja jina la hasimu wake Lionel Messi.
Kwa mujibu wa BBC. Baadhi ya mashabiki sasa wamekwenda hadi kwenye kampuni ya sheria mjini, inayofahamika kama Myungan kuwasilisha mashtaka.
Wanataka walipwe fidia ya won 70,000 (£48.50; $59) kwa kila tiketi , na milioni 1 ya fidia kwa kila mmoja kutokana na kile wanachokitaja kuwa “kuathirika kiakili “.
“Kwa kawaida katika hali kama hii mlalamikaji hulipwa gharama ya tiketi, lakini swala hili ninalichukulia kama swala la kipekee kwasababu kampuni , kupitia matangazo ya uongo, iliwalaghai mashabiki wa nyota huyo,” alisema wakili kutoka kampuni ya mawakili katika mazungumzo na shirika la habari la Reuters.
“Kwa upande wa tatizo la kuathirika kiakili , ningependa kusema kwamba baadhi yao ni mashabiki sugu, mashabiki sugu kabisa. Kwa hiyo kwao ni uchungu mkubwa kwasababu wanampenda Ronaldo na wanataka kumlinda, lakini hawawezi, kutokana na hali halisi ,” aliongeza.
“Kwa sasa tuna walalamikaji ambao waliishtaki kampuni , lakini nimekuwa nikipokea simu nyingi leo na ninadhani ni zaidi ya simu 60,000 .”
Robin Chang, Mkurugenzi mkuuu wa The Fasta, wakala wa Korea walioandaa mechi hiyo aliangua kilio mbele ya waandishi wa habari wa kampuni ya SBS na kuthibitisha kuwa mkataba ulieleza wazi kuwa Ronaldo angecheza kwa dakika 45.
Hata hivyo, Bi Chang alibaini tu kwamba mchezaji huyo wa miaka 34 hatacheza mechi dakika 10 tu baada ya kipindi cha pili.
“Nilipoenda kujaribu kuzungumza na (Pavel) Nedved, naibu rais wa Juventus, kile alichoniambia ni kwamba ‘pia mimi ningetamani Ronaldo acheze , lakini hataki kufanya hivyo . Samahani , hakuna ninaloweza kulifanya .’ Nilisikitika sana ,” alisema.
Shirika la soka la Korea Kusini Korea , K League, limesema kuwa barua ya kupinga tayari imetumwa kwa Ligi ya Championi ya Italia kwa kukiuka mkataba. Mashabiki wengi wamekuwa wakielezea hasira yao shisi ya Ronaldo kwenye mitandao ya habari ya kijamii.
“Amesaliti mashabiki 60,000 na kutudharau,” alisema mmoja wa mashabiki waliokuja kutazma mechi hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.