Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ametolea ufafanuzi kifo cha mtumishi wa Wizara ya fedha, Leopard Lwajabe (56), ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umening’inia kwenye mti wa muembe katika kijiji cha Mgoza wilayani Mkuranga.
Mambosasa amesema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa eneo la tukio hakukuwa na viashiria vyovyote vya kujitetea wakati wa tukio na kwamba mwili wa marehemu hakukuwa na jeraha lolote isipokuwa shingoni kulikokuwa kumefungwa kamba iliyotumika kujingonga.
Ametoa ufafanuzi huo leo Jumatano Julai 31, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema mnamo Julai 26 mwaka huu Polisi Kanda Maalum ya Rufiji walipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Mgoza, Mohamed Said (68), kwamba kumeonekana mwili wa mwanaume ukiwa unang’inia kwenye mti wa muembe na polisi walipofika waliukuta mwili huo ukionesha mhusika amenyinyonga.
“Julai 29, mwaka huu walipatikana ndugu wawili wa marehemu ambao ni Chumila Mwalimu mkazi wa Manyara na Jonathan Herman ambaye ni mfanyakazi mwenzake na marehemu ambao walifanikiwa kuutambua mwili na kueleza kuwa marehemu alitoka nyumbani kwake kwenda ofisini akiwa na dereva wake na baadae alimtuma dereva akamchukulie simu nyumbani kwake Kinyerezi na baada ya hapo marehemu alitoweka ofisini na kwenda kusikojulikana hadi alipogundulika amejinyonga,” amesema.
“Mnamo Julai 29, wafanyakazi waligundua kuwa marehemu aliacha notebook mezani kwake iliyokuwa na mgawanyo wa mali zake ambapo aliruhusu kati ya ng’ombe anaofuga wanne watumike katika msiba wake na pia simu aliyomtuma dereva iligundulika kuwa imeshafutwa kumbukumbu zote,” amesema.
Aidha amesema mwili wa marehemu ulihamishiwa hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi na ilibainika kifo hake kilisababishwa kwa kujinyonga ambapo chanzo hakijafahamika mpaka sasa na upelelezi uaendelea.
“Mtu aliyeuawa mahali halafu akaeda kufungwa kuna vitu vinavyokosekana kwa mfano mtu anayejinyonga lazima aachie haja ndogo na kubwa kwababu ya nguvu ya roho kutoka na hivyo vyote vimekutwa aneo la tukio,” amesema Mambosasa.
No comments:
Post a Comment