Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema amesema kuwa huenda IGP Simon Sirro ameona anapaswa kusimamia ukweli juu ya baadhi ya Makamanda wake kukiuka misingi na kujihusisha na vitendo vya siasa nchini.
Lema amesema hayo kufuatia kauli ya tahadhari ya IGP Sirro kwa Makamanda wa Polisi nchini wanaojihusisha na masuala ya siasa, lakini akihoji suala la vikao vya kinidhamu vya jeshi la Polisi na Makamanda wake wa nchi nzima kufanyika hadharani badala ya ndani.
"Naona IGP Sirro atakuwa ameona utendaji wake utakuwa mbaya akiachilia hili, kwa sababu bila Polisi imara taifa litaangamia au pengine amejua siku zake za kuwa kazini zinahesabika", amesema Lema alipozungumza na EATV & EA Radio Digital.
Ameendelea kusema kuwa hata baadhi ya makamanda katika mikoa hawaweki wazi na kuonyesha vitendo vya siasa lakini ndani yake kuna siasa wanazifanya kwa ndani.
Septemba 24 katika ufunguzi wa kikao cha Makamishina wa Polisi na Makamanda wa Mikoa, IGP Sirro alisema kuwa kulingana na amri za jeshi hilo, askari atakayejihusisha na siasa lazima wenzake watamshangaa, "changamoto ni baadhi yetu kujihusisha na siasa, katiba hairuhusu na kanuni za Polisi zipo wazi, polisi sio wanasiasa tujikite kwenye majukumu yetu".
"Watu wanataka kusikia unasema nini, wewe sio mwanasiasa unajiaibisha mwenyewe na unafanya hivyo kwasababu upo kwenye nafasi hiyo, tukikutoa hapo hutaweza kufanya, kuna watu wanatafuta umaarufu wa kisiasa tu", alisema Sirro.
No comments:
Post a Comment