Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kufuatilia utendaji kazi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah kwani hana ushirikiano mzuri na wafanyakazi walio chini yake.
Inaelezwa kuwa tangu Mkuu huyo wa Wilaya ahamie hapo, watumishi wengi wamehamishwa na wengine wakiomba kuhama kwa kile kilichoelezwa hana maelewano nao.
Waziri Mkuu ametoa maagizo leo Septemna 27, 2019, alipotembelea wilayani hapo ikiwa ni siku yake ya nne tangu alipoanza ziara ya kikazi mkoani humo na kubaini uwepo wa watumishi 14 wa ofisi hiyo, wakiwemo madereva 10 kuhamishwa baada ya Mkuu wa Wilaya kudai hawafanyi kazi ipasavyo.
“Lazima tuwatambue wasaidizi wetu na majukumu yao, ofisi ya Mkuu wa Wilaya haiwezekani ikawa hivi lazima kuna shida mpaka kufikia kuwaondoa watumishi wote. Mkuu wa Mkoa fuatilia hii ni mpya hapa tujue mbovu ni nani, tunataka tujue DC wako anataka dereva wa aina gani, tangu amefika hapa madereva 10 wote hawafai?'', amesema Waziri Mkuu.
Aidha katika hili Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa asipeleke watumishi wengine Wilayani hapo hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.
“Ili mfanye kazi vizuri mnatakiwa mshikamane, mfanye kazi kama timu moja kwani pamoja na shughuli mnazofanya hamna ushirikiano, DC sasa utabaki peke yako, utakuwa unaandika mwenyewe, unaendesha gari mwenyewe maana wote hawafai'', amesema Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment