UNAWEZA kusema ni kama hujuma, tangu mabosi wa Yanga walivyotua kwenye Mji wa Ndola nchini Zambia, ni kuwa umeme umekuwa ukikatwa kila mara na kusababisha mawasiliano kuwa magumu.
Viongozi hao wapo Ndola tangu Jumapili iliyopita na walitua mapema kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Zesco United ukiwa ni marudio ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo sehemu ya maandalizi ya viongozi hao ilikuwa kutengeneza mazingira mazuri kabla ya timu kuwasili nchini humo.
Kuelekea mchezo huo wa Raundi ya Kwanza utakaopigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela amesema kuwa maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri, licha ya kukutana na kasoro kadhaa likiwemo suala la umeme.
Mbali na umeme pia kumekuwa na tatizo la mtandao ambao umekuwa mgumu kupatikana kila wakati hali inayosababisha mawasiliano ya simu yasiwe mazuri wakiwa ndani na nje ya nchi.
“Tangu tumefika hapa kumekuwa hakuna huduma nzuri ya umeme maeneo mengi hata hotelini tulipofikia, kwani unapatikana kwa saa chache na ndiyo sababu unaona muda mwingine sipo hewani kutokana na simu kumalizika chaji. Tatizo hili limeendelea hata baada ya timu yetu kuwasili bado tatizo ni lilelile.
“Ninakuwa hewani pale simu inapokuwa na chaji pekee, hali hii inatutesa sana kwa kweli pia yapo matatizo mengine ambayo ni ya mtandao.
“Siyo muda wote mtandao unakuwepo hewani hali inayotufanya muda mwingine tushindwe kuwasiliana wenyewe kwa wenyewe tukiwa hapa Zambia,” alisema Mwakalebela.
Yanga inatakiwa ipate ushindi au sare ya zaidi ya bao 1-1 ili kusonga mbele, kufuatia sare ya 1-1 waliyoipata Uwanja wa Taifa, Dar katika mchezo wa kwanza.
No comments:
Post a Comment