ALIYEKUWA kocha wa timu ya Barcelona na timu ya taifa Hispania, Luis Enrique, amethibitisha kufariki dunia kwa mtoto wake wa kike Xana kutokana na kusumbuliwa na saratani ya mifupa.
Juni mwaka huu kocha huyo alitangaza kujiuzulu kuifundisha timu hiyo ya taifa Hispania baada ya kukosa kuisimamia kwenye michezo mitatu akidai alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya kifamilia.
Kutokana na hali hiyo Robert Moreno akapewa jukumu la kuchukua nafasi ya kocha huyo ndani ya timu ya taifa, lakini Rais wa shirikisho la soka Hispania aliwake wazi kuwa, milango iko wazi kwa kocha huyo akiwa tayari kutaka kurudi kikosini.
Juzi Enrique alitumia mitandao yake ya kijamii na kuthibitisha kufariki kwa mtoto wake huyo ambaye alikuwa na umri wa miaka tisa.
“Mtoto wetu wa kike Xana amepoteza maisha leo (juzi) huku akiwa na umri wa miaka tisa baada ya kupambana na saratani ya mifupa kwa miezi mitano.
“Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote ambao walikuwa na sisi katika kipindi chote cha miezi mitano ya kumuuguza mwanangu.
“Napenda kuwashukuru wafanya kazi wote wa hospitali ya Sant Joan de Deu na Sant Pau kwa kupambana kwao kwa ajili ya kupigania uhai wa mtoto wetu madaktari na manesi walikuwa pamoja nasi kila wakati hadi hatua za mwisho.
“Xanita tutakumisi sana na kukukumbuka kila siku hadi mwisho wa maisha yetu huku tukiamini mwisho wa siku tutakuja kukutana tena, ulikuwa ni nyota aliyokuwa inaing’alisha familia yetu, pumzika Xanita,” alisema Enrique.
Mastaa mbalimbali wa soka duniani wameshtushwa na taarifa hiyo, hivyo wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii na kutuma salamu za pole.
Miongoni mwa wachezaji hao ni pamoja na mshambuliaji wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Alvaro Morata, beki wa Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Nacho Fernandez, timu ya Barcelona, Real Madrid pamoja na chama cha soka nchini Hispania.
No comments:
Post a Comment