Mahakama ya Rufani imeanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Serikali, yenye mlengo wa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, iliyobatilisha sheria inayowapa mamlaka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia Uchaguzi Mkuu.
Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2018 ilifunguliwa na watetezi na wanaharakati wa haki za binadamu na demokrasia kwa kushirikiana na vyama vya siasa vilivyowakilishwa na mwanachama wa CHADEMA, Bob Chacha Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na kutolewa maamuzi Mei 10, 2019 na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Atuganile Ngwala.
Kufuatia maamuzi hayo, upande wa Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu ndipo walipoamua kukata rufaa.
Akizungumza leo Julai 30, Bob Chacha Wangwe amesema wamefika mahakamani hapo kwa lengo la kuanza kusikiliza rufaa hiyo, iliyo chini ya majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mziray, huku upande wa walalamikiwa ukiwakilishwa na mawakili takribani tisa wakiongozwa na Fatma Karume.
''Leo tumekuja kwa ajili ya kusikiliza rufaa, wenzetu upande wa Jamhuri na Tume ya Uchaguzi walikata rufaa baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu na mimi nawakilishwa na mawakili wasioupungua tisa wakiongozwa na Fatma Karume'', amesema Bob Wangwe.
Kufuatia rufaa hiyo Wangwe amesema, upande wao upo tayari kupokea maamuzi yatakayotolewa na Mahakama hiyo na kama hawajaridhika watakata rufaa.
No comments:
Post a Comment