Akizungumza jijini Mwanza leo Jumatatu Julai 8, 2019 katika ziara yake ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za polisi eneo la Myamhongolo, IGP Sirro ameuagiza uongozi wa jeshi hilo mkoani Singida kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyojeruhi wafanyakazi wengine wa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa uzalishaji vipindi wa kampuni ya Azam Media, Yahya Mohamed, waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea asubuhi ya leo ni Salim Mhando, Florence Ndibalema, Said Haji, Sylvanus Kasongo na Charles Wandwi.
Madereva wa Coaster lililokuwa limewapakia wafanyakazi 10 wa kampuni hiyo, pamoja na dereva wa lori pia wamefariki katika ajali hiyo iliyotokea wakati wafanyakazi hao wakiwa njiani kwenda wilaya ya Chato Mkoa wa Geita nchini Tanzania kuripoti tukio la uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Chato-Burigi.
Uzinduzi wa Hifadhi hiyo unatarajiwa kufanywa kesho Jumanne Julai 9, 2019 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli.
Awali akizungumza askari katika uwanja wa Polisi Mabatini jijini Mwanza, IGP Sirro alikemea tuhuma ya vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili miongoni mwa baadhi ya askari huku akionya kuwa atachukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya askari yeyote wa ambaye ushahidi dhidi yake utapatikana.
Kuhusu wimbi la wahamiaji haramu katika baadhi ya visiwa ndani ya Ziwa Victoria, Mkuu huyo wa jeshi la polisi aliwaagiza Makamanda wa Polisi katika mikao ya kanda hiyo kuendesha operesheni maalum kuwakamata na kudhibiti wahamiaji haramu.

No comments:
Post a Comment