KAZI imeanza. Unaambiwa huko Msimbazi mambo ni moto na hii ni baada ya mabosi ya timu hiyo kuwawahi Waarabu kwa kutuma jeshi lao michuano ya CAF, huku jina la Gadiel Michael nalo likiwemo baada ya beki huyo kubadili mawazo ya kwenda Sauzi.
Beki huyo aliyekuwa Yanga aliipotezea ofa ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa kilichoelezwa kuchanganywa na fedha alizomwagiwa na Simba na kusaini mkataba wa miaka miwili tofauti na kauli aliyoitoa awali kuwa, anataka changamoto mpya nje ya nchi.
Mwanaspoti linafahamu Gadiel mkataba wake na Yanga unamalizika Septemba mwaka huu na hicho kimewafanya mabosi wa Simba kushindwa kumtambulisha ikihofia yasije yakawakuta kama msala wa Hassan Kessy alipohamia Yanga.
Suala la Gadiel linafanana kama ilivyokuwa usajili wa Ibrahim Ajibu ambaye inaelezwa licha ya kusaini mapema, lakini ilisubiriwa mkataba wake na Yanga umalizike rasmi Juni 30 ndipo alipotangazwa akiwa mmoja ya nyota watakaokinukisha msimu ujao.
Licha ya mabosi wa Simba kufanya siri kubwa, lakini inadaiwa, jina la Ajibu na Gadiel ni kati ya nyota 25 wa Simba waliopelekwa ofisi za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wakifanya hivyo kuwahi tarehe ya mwisho ya usajili bila faini iliyotangazwa.
CAF iliweka mpaka Julai 10 klabu shiriki za michuano yake ya msimu wa 2019-2020 kufanya usajili na baada ya hapo ikisajili italazimika kulipa faini ya Dola 250 kwa siku 10 na Dola 500 kwa siku 11 za ziada na Simba imeona isiwe tabu kutangaza jeshi lake mapema.
Inaelezwa mabosi wa Simba baada ya kukamilisha usajili wa Gadiel waliwasiliana na Kocha, Patrick Aussems aliyepo mapumzikoni naye akaridhia majina yatumwe CAF na kama kuna nafasi za kuongezwa basi wataufanya baadaye.
Kwa mujibu wa chanzo makini kutoka Simba majina yaliyotumwa CAF ni pamoja na makipa Aishi Manula, Benno Kakolanya na Ally Salim, huku mabeki wakiwa ni Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Tairone Da Silva, Yusuf Mlipili, Gadiel Michael, Kennedy Juma na Gerson Fraga Vieira.
Huku, Msudan Shiboub Sharaf eldin, Francis Kahata, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Clatous Chama wakiunda safu ya viungo, huku washambuliaji wakiwa ni pamoja na nahodha John Bocco, Rashid Juma, Wilker Henrique da Silva, Ibrahim Ajibu, Deo Kanda, Miraj Athuman na Meddie Kagere.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba Mulamu Ng’hambi aliyekuwa akishughulika na ishu za usajili wa klabu hiyo CAF kwa msimu uliopita juu ya jeshi hilo jipya, alisema hajui chochote kwa vile zoezi hilo kwa sasa linafanywa na mtu mwingine. Naye Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu alisema bado hawajamaliza usajili, wataongeza nyota wapya wawili au watatu lakini watajitahidi kuwahi kabla ya Julai 10.
“Tukikamilisha usajili mtatangaziwa, kuna nafasi za kuogezwa na tunadhani tutawahi kutuma majina CAF na tunaangalia jinsi ya kuziba nafasi zitakazosalia,” alisema Rweyemamu.
“Kuna kiongozi ndiye anayekamilisha zoezi hilo ila kama kutakuwa na mabadiliko ya wachezaji wengine kuingia au kutoka mtajulishwa.”

No comments:
Post a Comment