Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai huenda ndiye kiongozi wa Mhimili pekee ambaye amekuwa akiingia kwenye migogoro ya mara kwa mara na baadhi ya Wabunge, pamoja na viongozi wengine wa Serikali kutokana na sababu mbalimbali.
Www.eatv.tv imekukusanyia baadhi ya migogoro ambayo kiongozi huyo wa Mhimili wa Bunge amekuwa akihusishwa nayo, na mengine kuishia kwa baadhi ya viongozi kuitwa kamati ya maadili au kuishia kwenye mrushiano wa maneno.
June 2019, wakati timu ya Taifa ya Tanzania ikiwa nchini Misri ikicheza mchezo wake dhidi ya timu ya Taifa ya Senegal ambapo ilipoteza kwa mabao 2 -0, aliporudi nchini Spika Ndugai akiambatana na Wabunge alitoa kauli ambayo ilimuingiza kwenye mrushiano wa maneno na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, ambapo yeye alidai kuwa wachezaji wa Tanzania hawakuwa na lishe.
Baada ya Mkuu Mkoa Dar es salaam kueleza masikitiko yake kwenye uzinduzi wa ghala la kuhifadhia gesi Kigamboni jijini Dar es salaam mbele ya Rais Magufuli, Spika Ndugai alimjibu tena Makonda kupitia vikao vya Bunge vilikuwa vikiendelea jijini Dodoma.
Mei 2019, Spika Ndugai tena aliingia kwenye mgogoro na Mbunge wa Kahama Mjini Stephen Masele, baada ya Spika Ndugai kudai kuwa alimuita Masele arudi Tanzania kwa ajili ya kujieleza lakini Stephen Masele alikaidi wito huo, na kudai ulikuwa ni mpango wa Rais wa Bunge la Afrika ambaye kwa wakati huo alikuwa akituhumiwa kwa utovu wa maadili.
Mgogoro uliisha baada ya Masele kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Bunge kuridhia kumsamehe.
April 2019, Ulikuwa ni muendelezo wa mgogoro baina ya Spika Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG, kuhusiana na kauli ya kuwa ni Bunge ni dhaifu na mgogoro uliishia baada ya Bunge kuazimia kutofanya kazi na Prof Mussa Assad.
Jan 2019, pia ulikuwa ni muendelezo wa mgogoro wa kurushiana maneno baina ya Spika Ndugai na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, kuhusiana na gharama za matibabu za Mbunge huyo ambaye alishambuliwa kwa risasi Septemba 07, 2017 akiwa Bungeni jijini Dodoma.
Novemba 2018, Spika Ndugai alisoma orodha ya majina ya Wabunge na Mawaziri ambao walikuwa na mahudhurio hafifu ndani ya Bunge huku akimtaja Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuwa anaongoza kwa mahudhurio hafifu ndani ya Bunge, hali ambayo ilimuibua Mbunge Lema na kueleza anajivunia kutoingia Bungeni kwa alichokidai kuwa Bunge limepoteza mvuto.
Chanzo: EATV
No comments:
Post a Comment