Idadi ya vijana na watu wazima wenye umri chini ya miaka 45 wanaopata ugonjwa wa kiharusi imezidi kuongezeka, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Matokeo ya utafiti huo uliofanywa kati ya Juni 2018 na Januari 2019 yaliwasilishwa juzi kwenye Mkutano wa Saba wa Sayansi chuoni hapo. Utafiti huo ulitokana na wagonjwa waliopatiwa matibabu katika kituo cha tiba kilicho ndani ya Muhas.
Ilibainika kuwa wagonjwa 123 kati ya 369 waliobainika kuwa na kiharusi ni vijana na watu wazima wenye umri chini ya miaka 45; na wengine 246 ni watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 45 pamoja na wazee.
Kiongozi wa utafiti huo, Dkt. Sarah Matuja alieleza kuwa ugonjwa wa kiharusi huaminika kuwa unawapata zaidi wazee lakini utafiti huo umeonesha kuwa vijana wengi pia wako hatarini.
Alisema kuwa chanzo kikuu cha kiharusi kinaaminika kuwa ni shinikizo la damu (blood pressure), na kwamba wagonjwa wengi waliotibiwa katika kituo hicho walikuwa na shinikizo la damu.
Aidha, alisema kuwa vijana wengi waliokutwa na shinikizo la damu hawakuwa wanajua kama wana tatizo hilo hadi walipopima wakati huo wakiwa na kiharusi, tofauti na wazee ambao mara nyingi hupata vipimo vya shinikizo la damu.
Wataalam wa tiba wameeleza kuwa vitu vinavyowafanya vijana kuwa katika hatari zaidi ya kupata kiharusi ni ulevi wa pombe, Virusi Vya Ukimwi, ugonjwa wa moyo na mengine.
Kwa mujibu wa Dkt. Matuja, kiharusi kinaweza kudhibitiwa kwa kuhakikisha hauna uzito kupita kiasi, hauna shinikizo la juu la damu na kufanya mazoezi mara kwa mara.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la kiharusi kwa vijana na watu wazima, ambapo mtu mmoja kati ya sita wanaopata kiharusi ni kijana/mtu mzima mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 50.
No comments:
Post a Comment