Viongozi mbalimbali wa taasisi, vyama na klabu za michezo, wameungana na Watanzania kote nchini katika kuombeleza kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dr. Reginald Mengi kilichotokea usiku wa kuamkia leo katika Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E).

Mratibu wa klabu ya Yanga, Hafidh Saleh, amesema, "tumepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mzee wetu Reginald Abraham Mengi, tutamkumbuka kwa mengi sanan kwenye sekta yetu ya michezo. Sisi kama Yanga tunamlilia sana kwa sababu alikuwa ni kiongozi ambaye anatusaidia sana, huko nyuma alishawahi kuhusika katika kutatua mgogoro ambao ulidumu kwa muda mrefu na mambo mengine mengi ametusaidia kama mwanachama mwenzetu".
Moses Mabula, ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu TAFF, ametoa salam kwa niaba ya Shirikisho akisema, "tumepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Dr. Mengi, kama tunavyofahamu, alijitoa sana kusaidia jamii ya watu wenye ulemavu na sisi kama shirikisho hatutoacha kumkumbuka kwasababu alikuwa ni mlezi wetu kwa kipindi fulani. Aliahidi kutusaidia kwa mambo mengi sana hasa kuelekea katika mashindano Afrika Mashariki na Kati kwa Watu wenye Ulemavu".
Naye, Meneja wa klabu ya Azam FC, Philipo Alando, amesema, "ni masikitiko makubwa kumpoteza Dr. Reginald Mengi, ninamkumbuka kwa sapoti yake kubwa katika tasnia ya michezo hasa kwa kuzisapoti timu za taifa za vijana, tunapenda kutoa pole kwa EATV na EA Radio, ITV na Radio One, pamoja na makampuni yote ya IPP, familia na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huu mzito".
No comments:
Post a Comment