Taasisi ya Ustawi wa Jamii, imetakiwa kusogeza huduma karibu zaidi kwa Wananchi kwa kufungua matawi katika kila kanda, ikiwemo vyuo vinavyotoa Elimu kuhusu Ustawi wa Jamii,
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu jana katika uzinduzi wa bodi ya tano ya magavana ya taasisi ya ustawi wa jamii Jijini Dar es salaam.
Waziri Ummy amesema kuwa ni lazima Taasisi hiyo kuweka mpango mkakati wa kuhakikisha unasogeza huduma za Ustawi wa Jamii kwa kujenga Matawi katika kila Kanda ili kuepusha usumbufu wakufata huduma hizo Jijini Dar es salaam.
“Ni lazima tusogeze huduma hizi za taasisi kwenye kanda, tuweke kwenye mpango mikakati yetu kwamba ndani ya miaka mitano tuwe na matawi angalau kanda mbili, kwanini watu waje kupata huduma Dar es salaam jambo ambalo linapelekea usumbufu”, amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa jumla ya wataalamu 9,140 wa Ustawi wa Jamii na Taaluma zinazoelekea Ustawi wa Jamii wamezalishwa nchini huku Idadi hii ikiwa ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya Maafisa Ustawi wa Jamii 23,694 wanaohitajika jambo lililopelekea huduma kutolewa chini ya kiwango.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa ni jukumu la kila mtu kuhakikisha kuwa Taasisi ya Ustawi wa Jamii inashiriki na kutoa mchango wake makhususi katika kuimarisha Taaluma ya Ustawi wa Jamii kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano katika kuelekea uchumi wa viwanda.
No comments:
Post a Comment