Klabu ya soka ya Yanga jana April 29, 2019, imeibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Azam FC, ushindi ambao umeendelea kuwaweka kileleni mwa ligi kuu, lakini msemaji wa Simba Haji Manara amewaambia hawana nafasi ya ubingwa.
Akieleza maandalizi ya mchezo wa Simba dhidi ya JKT Tanzania jana, Manara amesema Simba ndio mabingwa na tayari ubingwa wa ligi kuu upo mikononi mwao.
''Sisi ni bingwa wa taifa hili na ubingwa wa msimu huu upo milkononi mwetu, yaani kila mtu akishinda zake tutakaa juu kwa pointi kumi'', amesema Manara.
Aidha Manara amesema wanachotakiwa kufanya Yanga ni kuendelea kushinda mechi zao, na Simba nao washinde mechi zao na baadae wapige hesabu na kuona nani atakuwa zaidi ya mwenzake.
Manara amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwenye uwanja wa Uhuru ili kuipa nguvu timu yao.
Simba ipo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 69 katika mechi 27 wakati Yanga wanaongoza ligi wakiwa na pointi 77 katika mechi 33. Endapo timu zote zitashinda mechi zilizobaki Simba watakuwa na pointi 102 wakati Yanga watakuwa na 92.
No comments:
Post a Comment