SIMBA Wamebakiza pointi tano tu wawang’oe wapinzani wao Yanga katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo. Sasa ili kukoleza vita ya kuwashusha, nyota wa kikosi hicho kilicho chini ya uwekezaji wa bilionea kijana Mohamed Dewji ‘Mo’, leo Jumatatu watapewa kiasi cha Sh milioni 240 kwa ajili ya kuongeza motisha.
Simba walipata pointi tisa katika mechi nne walizocheza Kanda ya Ziwa, ambapo Emmanuel Okwi na John Bocco walikuwa nguzo kwenye upatikanaji wa pointi hizo huku kila mmoja wao akiweka kambani mabao matatu. Simba kwa sasa wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 69, zikiwa ni pointi tano nyuma ya Yanga ambao wapo kileleni wakiwa na pointi 74.
Chanzo kutoka ndani ya Simba kimeliambia Championi Jumatatu, kuwa kiasi hicho cha Sh milioni 240 watakachopewa kwa ajili ya kuongeza upambanaji wa kusaka ubingwa kinatokana na ushindi wa michezo minne kati ya mitano iliyopita.
“Kuanzia kesho (leo) Jumatatu, wachezaji watawekewa fedha zao za bonasi baada ya kushinda mechi nne. Kila mechi ambayo wameshinda walitakiwa kupewa Sh milioni 60, maana yake kushinda mechi nne watachukua Sh milioni 240.
“Wamechelewa kupewa fedha kwa sababu viongozi walikuwa na timu huko Kanda ya Ziwa pamoja na baadhi ya watu wa fedha, ndiyo maana ikachelewa lakini kuanzia kesho (leo) kila kitu kitakuwa sawa.
“Kikosi kimerudi leo Jumapili (jana) kwa ndege kwa ajili ya kujiandaa na mechi nyingine baada ya kumaliza kazi kule Kanda ya Ziwa na kupata pointi tisa,” kilisema chanzo hicho.
Simba walipata ushindi kwenye mechi tatu za Kanda ya Ziwa dhidi ya Alliance (2-0), KMC (2-1) na Biashara United (2-0) lakini pia walishinda mechi nyingine dhidi ya Coastal Union ya Tanga mabao 2-1, huku wakifungwa na Kagera Sugar 2-1.
Championi Jumatatu, lilimtafuta Mratibu wa Simba, Abass Ally, ambapo alisema: “Kila kitu kuhusiana na timu ni mpaka turudi Dar, kwa sasa hatuwezi kuzungumzia chochote.”
No comments:
Post a Comment