Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Kampuni ya Sport Pesa wamethibitisha kuwa mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC watacheza na mabingwa wa kihistoria wa Europa League, Sevilla FC ya Hispania, Mei 23, 2019 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Awali kulikuwa na mkanganyiko kuwa kati ya Simba na Yanga nani acheze na Sevilla kabla ya leo TFF kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo.
Katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidao amesema kigezo cha kuichagua Simba kucheza na Sevilla ni sababu ya kumaliza nafasi ya juu dhidi ya Yanga katika michuano ya SportPesa, ambayo ndio wanaoileta timu hiyo hapa nchini.
“Sasa ni rasmi Simba ndio itacheza na Sevilla katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Mei 23, 2019, kwakuwa ndio walifika nusu fainali kwenye michuano ya SportPesa iliyofanyika nchini mwezi Januari mwaka huu pia hii ni kwasababu ratiba ya ligi haikuwa rafiki kwa kucheza mechi ya kumtafuta mshindi kati ya Simba na Yanga,” alisema Kidao.
Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbas amewataka Simba kujiandaa vizuri kuelekea mchezo huo ili kulitangaza soka la nchi kwakuwa mechi itatangazwa kote duniani.
No comments:
Post a Comment