Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imepigilia msumari nia yake ya kukichukulia hatua za kisheria Chama cha ACT-Wazalendo ikiwa zimebaki siku nane tangu kipewe siku 14 kuwasilisha maelezo ya kwa nini kisifutiwe uanachama wa kudumu.
Akizungumza na Mwananchi, msajili msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema endapo chama chochote kitakiuka sheria, hawatasita kutoa adhabu huku akibainisha kuwa wamekuwa wakivionya na kutoa adhabu mara kadhaa kwa vyama mbalimbali na siyo ACT pekee.
Machi 25, ofisi hiyo ilieleza nia yake ya kutaka kukifutia usajili chama hicho na kukipa siku 14 kuanzia Machi 26 kuwasilisha maelezo ya kwa nini kisifutwe uanachama wa kudumu.
Hatua hiyo ilikuja ikiwa imepita wiki moja tangu aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na ACT akiwa pamoja na waliokuwa viongozi waandamizi wa chama hicho na wanachama wa kawaida.
Barua hiyo ilieleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, msajili wa vyama anapotaka kufuta usajili wa chama cha siasa anapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa chama hicho.
Imeyataja mambo yanayodaiwa kukiukwa na chama hicho kuwa ni vitendo vya uvunjifu wa sheria vya kuchoma moto bendera za CUF baada ya Mahakama Kuu kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016.
Mahakama ilimtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF.
Pia, chama hicho kinatuhumiwa kutumia udini baada ya mashabiki wake kuonekana mitandaoni wakipandisha bendera ya ACT Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbir), kitendo kinachodaiwa kukiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.
Mbali na hatua hizo, ofisi ya msajili imesema chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 kinakabiliwa na adhabu nyingine ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/2014.
Katika mahojiano maalumu, Nyahoza alilieleza Mwananchi wiki hii kuwa si mara ya kwanza vyama vya siasa ikiwamo ACT kukutana na barua za kujieleza kutokana na ukiukwaji wa sheria.
Alisema Novemba 2016, ofisi hiyo ilitangaza nia ya kuvifuta vyama 11 na vilipewa barua za kujieleza kwa nini visifutiwe usajili kutokana na ukiukwaji wa sheria kwa makosa mbalimbali likiwamo la kutowasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha.
Katika uamuzi huo, vyama vya Chausta, APPT-Maendeleo na Jahazi Asilia vilifutiwa usajili.
“Mwaka 2016 ulisikia kuna chama kimeenda kutujibu kwenye media? (vyombo vya habari?)Hawakwenda. Walijibu na tulipoona wame-clear (wameweka mambo sawa) tukaachana nao. Sasa utaratibu wa kiofisi tumewaandikia barua (ACT), wanatakiwa watujibu kwa barua, vinginevyo utaona muda ukifika tutachukua hatua,” alisisitiza Nyahoza.
Nyahoza alisema Machi mwaka jana, ofisi ya msajili ilisitisha ruzuku kwa ACT-Wazalendo na chama hicho kilitakiwa kuwasilisha maelezo baada ya kuvunja sheria kwa kutowasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu zake kwa mwaka 2013/2014.
Maalim Seif si chanzo
Alipoambiwa kuna madai kuwa kuhamia ACT kwa Maalim Seif kuwa ndicho chanzo cha mambo yote hayo, Nyahoza alisema hayana ukweli wowote.
“Tulianza kuwapa adhabu ndogondogo (ACT - Wazalendo) tukawaambia wajirekebishe, tangu mwaka jana kipindi kama hiki tuliwapa notice, tukawaambia jamani eeh tuna nia ya kuwachukulia hatua, rekebisheni masuala ya hesabu, tukawafungia ruzuku, lakini mpaka sasa hivi hawajajirekebisha, ni mwaka mzima. Kwa hiyo kama hawatatekeleza kweli kabisa tutawamwaga tu.”
“Tutawaambia wananchi sisi hatuonei mtu, hayo masuala ya Maalim Seif hatunayo, tumeanza mapema sana kushughulika na ACT-Wazalendo, tena tulikuwa tunashangaa Zitto (Kabwe) aliyekuwa mwenyekiti wa PAC (Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali), anajua umuhimu wa hii kitu, utachelewaje kukileta? (taarifa ya hesabu). Sasa yeye anapata ruzuku je kwa vyama visivyokuwa na ruzuku vifanyeje?” alihoji Nyahoza.
CCM imewahi kuonywa
Nyahoza alisema hakuna upendeleo wala uonevu kwa vyama vya siasa nchini kwa kuwa vyote viko chini ya sheria.
“Hata CCM tuliwahi kuwaandikia barua ya onyo baada ya kuonekana wakifanya kampeni na yule Rais wa China, tulitoa press release (taarifa kwa vyombo vya habari), kwa hiyo hatuna upendeleo,” alisema.
Zitto ajibu
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu mchakato wa kuwasilisha utetezi wao, Zitto alisema wameshakamilisha maelezo wanayotakiwa kuyawasilisha kwa msajili na watafanya hivyo ndani ya muda waliotakiwa.
Machi 26, Zitto katika mkutano wake na waandishi wa habari alizijibu hoja tatu zilizowasilishwa na msajili.
Kuhusu ukaguzi wa hesabu alisema waliwasilisha hesabu za mwaka 2013/14.
“Chama chetu kilianzishwa na kupata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 ikiwa ni miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha kuisha yaani Juni 30, 2014,” alisema
“Kwa kutumia kanuni za kimataifa za hesabu na kwa ushauri wa CAG, chama chetu kilielezwa kinaweza kuunganisha hesabu za mwaka 2013/14 na za 2014/15 katika ripoti moja, hili ni jambo la kawaida kabisa katika kanuni za uhasibu, inaruhusiwa kuunganisha hadi miezi 18.”
Alisema kabla ya kufanya hivyo, walimwandikia msajili wa vyama vya siasa barua mbili ya Januari 22 na 29, 2015 naye akajibu kuridhia hesabu hizo kuunganishwa kwenye barua ya Februari 16, 2015.
Kuhusu kuchoma bendera za CUF alisema, “msajili alipaswa ajiridhishe anaowatuhumu ni wanachama wa ACT Wazalendo, kabla ya kutuandikia barua. Nina uhakika hawezi kwenda mbele ya mahakama kuthibitisha hilo.”
Kuhusu kutumia neno Takbir, alisema Katiba na kanuni za chama hicho zinaonyesha wazi kuwa hawafungamani na dini yoyote ndio maana wameruhusiwa kufanya shughuli za siasa.