Kikosi cha Simba kimeendelea kujifua nchini Misri kujiandaa na mchezo wa kesho wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly
Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema tangu watue Misri siku mbili zilizopita, wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakijifua bila hofu, morali yao iko juu huku kila mmoja akiwa na shauku ya kupata matokeo mazuri kesho
Kuhusu hali ya baridi Rweyemamu wamesema walifahamu wangekutana na hali hiyo hivyo walijipanga kabla ya kuanza safari. Anaamini haiwezi kuwa changamoto kwa wachezaji katika mchezo huo
"Tunaendelea vema, programu yetu ya mazoezi ni mara moja tu, jana (juzi) tulifanya usiku na leo (jana) pia tutafanya mazoezi usiku kuanzia saa 1:30 ya huku, ila tumetafuta uwanja mwingine na si ule utakaotumika Jumamosi," alisema Rweyemamu.
"Kuhusu baridi isiwatie hofu, tunafahamu hali hii, kwa sasa (jana mchana) wachezaji wamepumzika, hadi sasa wote ni wazima jambo ambalo tunaendelea kumshukuru Mungu," aliongeza meneja huyo.
Naye kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems alizungumzia maandalizi ya mchezo huo ambapo alisema muitikio wa wachezaji ni mzuri na hana wasiwasi watafanya vizuri kesho.
"Tayari nimewaelekeza nini wanapaswa kufanya na nini wasifanye. Nafurahi wamekuwa na muitikio mzuri katika mazoezi ninayowapa"
Mchezo dhidi ya Al Ahly utapigwa kesho Jumamosi, Februari 02 2019 saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki na utarushwa mbashara na chaneli za ZBC 2 na SS4 vin'gamuzi vya Azam na DSTV
No comments:
Post a Comment