Kuelekea mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kati ya Yanga na Polisi Tanzania, Msemaji na Afisa Muhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz amesema kuwa sasa wamerejea rasmi katika ligi na watatembeza kichapo kwa yeyote atakayetokea.
Akizungumza na EATV&EA Radio Digital katika Makao Makuu ya Klabu hiyo, Nugaz amesema kuwa kesho Alhamisi, mashabiki wa Yanga wantakiwa kuja kufurahi uwanjani kwakuwa kazi waliyonayo hivi sasa ni kukusanya kila pointi tatu zilizo mbele yao.
"Polisi Tanzania tulishawahi kucheza nao mechi ya kirafiki na tukapoteza dhidi yao, lakini wajue kabisa unapokuwa na Yanga mashindanoni ni tofauti kabisa unapocheza nayo kirafiki, hilo walizingatie", amesema Nugaz.
"Tunataka mashabiki wetu wafike uwanjani kusapoti timu yao, kesho tumejipanga kupambana kuhakikisha kila anayeshuka Dar es Salaam na hata nje ya Dar es Salaam tunachukua pointi tatu kuhakikisha tunarudi kileleni ambako Yanga inastahili kukaa", ameongeza.
Yanga ilipoteza mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting kwa bao 1-0 na sasa iko katika nafasi za mwisho za ligi, ikiwa imecheza mchezo mmoja pekee.
No comments:
Post a Comment