Mtu mmoja amezama na mtumbwi katika Ziwa Momella, lililopo katika mbuga ya Arusha, baada ya mtumbwi aliokuwa nao kupigwa na dhoruba, iliyosababishwa na kimbunga kikubwa kilichozua taharuki kwa wakazi wa mkoa huo siku ya jana.
Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, leo Oktoba 2, 2019, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Koka Moita, amesema kuwa mtu huyo anadaiwa kuzama majira ya saa 9:00 jioni siku ya Oktoba 1, lakini licha ya jitihada za uokozi kufanyika hawakuweza kumpata.
''Wilaya ya Arumeru katika mbuga ya Arusha ndani ya ziwa Momella, kulikuwa na watalii wawili waliokuwa wamekodisha mitumbwi, upepo ulivyokuja ulileta dhoruba na mitumbwi ikaanza kuyumba, lakini mtumbwi mmoja uliweza kutoka salama lakini yule nahodha wa mtumbwi wa pili ambaye ni mtanzania alizama na siku ya jana hatukufanikiwa kumpata'', amesema Kamanda Moita.
Kamanda Moita ameongeza kuwa juhudi za kumuokoa mtu huyo zinaendelea kwa kushirikiana na Jeshi la polisi, TANAPA pamoja na Jeshi la Zimamoto na uokoaji.
No comments:
Post a Comment