Na Zuena Msuya, Morogoro,
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, ameagiza Afisa aliyekuwa akisimimamia Mradi wa Umeme Vijijini (REA), Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Seif Abdallah, aondolewe kwenye nafasi hiyo kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
Aidha Dkt. Kalemani ametoa siku 20, kwa Kampuni ya Ukandarasi ya State Grid inayotekeleza mradi huo kuwasha umeme katika vijiji vya Wilaya ya Ulanga la sivyo atakatwa asilimia kumi ya malipo yake kutokana na kazi hiyo.
Dkt.Kalemani alitoa kauli hiyo Agosti 31,2019, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa REA na kuwasha umeme katika Vijiji vya Makanga na Idunda wilayani Ulanga, mkoani Morogoro.
Waziri wa Nishati alifikia hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na usimamizi unaofanywa na mhandisi huyo kutoka Wakala wa Nishati Vijiji ( REA) pamoja na utekelezaji wa mradi usioridhisha.
“Huyu Mhandisi Seif Abdallah, utendaji wake wa kazi hauridhishi kabisa, hayupo katika maeneo ya kazi yanayotekelezwa mradi, anamuacha mkandarasi afanye kazi anavyojitakia yeye mwenyewe hakuna usimamizi wowote, ninamuagiza Mkurugenzi wa REA amuondoe huyu mhandisi hafai kuwa msimamizi”,alisisitiza Dkt.Kalemani.
Katika hatua nyingine, Dkt.Kalemani alitoa siku 20 kuanzia, Septemba 1 hadi 20, 2019 kwa kampuni ya ukarandari ya State Grid kuwasha umeme katika vitongoji vinne kabla ya kukamilisha Mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza unaotarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu nchini kote.
Alifafanua kuwa, utekelezaji wa Mradi wa REA awamu ya tatu umegawanyika katika mizunguko miwili ambayo ni mzunguko wa kwanza ulioanza kutekelezwa mwezi Juni, 2019 na utakamilika Desemba mwaka huu.
Aidha mzunguko wa pili wa REA awamu ya tatu unatarajiwa kuanza mwezi Januari na kukamilika mwezi Juni ,2020, hivyo alimtaka kila mkandarasi aliyepew kazi ya kutekeleza mradi huo ahakikishe anakamilisha mzunguko wa kwanza wa kazi yake kwa mujibu wa makubaliano ya mikataba na sheria.
Alisisitiza kuwa haridhishwi na hatua ya utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Morogoro ambao mpaka sasa umefikia asilimia 56 tu ya utekelezaji wake ambao hauendani na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.
Sambamba na hilo alimtaka mkandarasi huyo,kuongeza nguvu kazi ya makundi ya vijana ili kuharakisha shughuli za utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza kama ilivyoelekezwa katika mkataba wa kazi hiyo.
“Sitakubali kukwamishwa na ninyi State Grid katika utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa mnafanya kazi kwa kusuasua sana kasi yenu hairidhishi kabisa, na nyie ndiyo mko nyuma kabisa katika kasi ya kutekeleza mradi wa huu REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza ikilinganishwa na wakandarasi wote wanaotekeleza miradi hii nchini, kama hamtatimiza makubaliano ya mkataba, tutawakata asilimia 10 ya malipo yenu”, alisema Dk.Kalemani.
Hata hivyo, Dkt.Kalemani alirejea kauli yake ya kuwataka wananchi kuwa wasinunue miundombinu ya umeme kama vile nguzo, pamoja Luku kwa kuwa vifaa hivyo vinatolewa bure kwa kila mwananchi aliyepitiwa mradi wa umeme vijijini.
Pia aliwataka wananchi kutumia umeme kwa faida kama vile kuongeza thamani ya mazao kwa kufanya usindikaji wa mazao yao ili kujiletea maendeleo zaidi.
Serikali imetenga shilingi Bilioni 42 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza kwa Mkoa wa Morogoro.
No comments:
Post a Comment