Mshambuliaji wa Yanga Juma Balinya amesema wana kazi ya kuhakikisha wanapata matokeo yatakayowapeleka hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Zesco United
Kesho Jumamosi, Yanga itakuwa ugenini uwanja wa Levy Mwanawasa kuikabili Zesco United katika mchezo wa marudiano
Wiki mbili zilizopita, timu hizo zilikutana jijini Dar es salaam na Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1
Ni mchezo ambao Yanga inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao mawili ili iweze kutinga makundi
Aidha matokeo ya sare ya bao 1-1 yataupeka mchezo huo hatua ya mikwaju ya penati wakati suluhu ya bila kufungana itaiondosha Yanga kwenye michuano hiyo na kuipeleka kombe la Shirikisho
Balinya aliyekosa mchezo wa kwanza, anatarajiwa kuanza kwenye mchezo huo baada ya kuimarisha kiwango chake siku za karibuni
Kinara huyo wa mabao ligi kuu ya Uganda msimu uliopita, amesema wanahitaji kushinda kwa njia yoyote ili waweze kusonga mbele
"Tumefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo dhidi ya Zesco. Tunajua, tunahitaji kushinda.. Tunahakikisha tunalikamilisha hilo kwa namna yoyote," amesema
Jana jioni Yanga ilijifua katika uwanja maalum wa mafunzo ambao walipewa idhini ya kuutumia na chama cha soka cha Zambia
Leo mabingwa hao wa kihistoria watajifua katika uwanja wa Levy Mwanawasa ambao utatumika kwenye mchezo huo kesho
No comments:
Post a Comment