Kaka wa marehemu Nelson Olotu aliyefariki baada ya kupata ajali ya ndege ndogo, ajulikanaye kwa jina la Kelvin Olotu, ameeleza historia fupi ya mdogo wake wakati wa ibada ya mazishi na kusema kuwa Nelson alikuwa na ndoto kubwa, ambayo isingeweza kuzimwa na mtu yeyote.
Ibada ya mazishi ya Nelson imefanyika leo Septemba 27, 2019, katika kanisa la KKKT Wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro na kusema kuwa mdogo wake alikuwa na ndoto ya muda mrefu licha ya wazazi kumshauri ajikite kwenye uhandisi wa ndege na aachane na urubani, kutokana na ajali kadhaa ambayo waliwahi kuisikia na kuwatia hofu.
''Alikuwa akiwaeleza Mama na Baba, mimi ndoto yangu nikuwa Rubani na sitachagua kitu kingine chochote cha kufanya kwenye maisha yangu,kwahiyo hiyo ndo njia yangu iliyopo na ninaomba ninyi kama wazazi mnatakiwa mnisaidie na kunishika mkono” amesema Kelvin.
Kijana Nelson Olotu alifariki Dunia Septemba 23, 2019 baada ya ndege ya kampuni ya Auric Air waliyokuwa wakiendesha, kupata hitilafu na kuanguka katika kiwanja kidogo cha ndege cha Seroneru, kilichopo katika hifadhi ya taifa ya Serengeti mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment