Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping amemtunuku Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Dkt. Salim Ahmed Salim, nishani ya juu ya urafiki kati ya Mataifa haya mawili, ambapo mtoto wake wa kike Maryam Salim amepokea nishani hiyo kwa niaba ya baba yake (Dk. Salim).
Dkt.Salim ametunukiwa nishani hiyo kutokana na mchango wake uliowezesha Jamhuri ya Watu wa China (PRC) kurejesha kuwa mwanachama wa kudumu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971, alipokuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN).
Dkt. Salim alikuwa Waziri Mkuu tangu mwezi Aprili 1984 hadi Novemba 1985, akiwa Waziri Mkuu wa tano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufuatiwa na Joseph Sinde Warioba, Mpaka leo Dkt Salim ndiye Mtanzania wa kwanza mwenye umri mdogo kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nje ya nchi, nakufanya kazi katika nchi za Misri, India na China.
Miongoni mwa majina yaliyotolewa na Sheikh Karume kwa Mwalimu Nyerere ni Dkt. Salim ambapo alikuwa na umri wa miaka 22, jambo ambalo lilimfanya Mwl, Nyerere kumuulizia mara ya pili Rais Karume juu ya umri wa kijana huyo, na majibu aliyopewa ni kuwa huyo ni kijana wa Zanzibar mwenye vigezo na uwezo hivyo apewe nafasi, na akateuliwa kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Uarabu ya Misri.
Mwaka 1976 alihudumu kama Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa United Nations Security Council (UNSC) na 1979 kama Rais wa Kikao cha 34 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lakini pia alikuwa kama Katibu Mkuu wa Iliyokuwa Jumuiya ya Muungano wa Afrika OAU.
No comments:
Post a Comment