Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya Watendaji Kata na askari nchini ambao wamekuwa wakishindwa kuzifikisha sehemu husika kesi za watu, waliowapa ujauzito wanafunzi na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ameyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilula Sokoni, kata ya Nyalumbu wilayani Kilolo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.
"Wanafunzi bado wanaendelea kupewa ujauzito na kukatishwa masomo yao huku watu waliohusika na vitendo hivyo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa sababu baadhi ya watendaji na askari wamezikalia kesi zao na kushindwa kuwafikisha polisi", amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa na kulindwa katika jamii, lengo likiwa ni kumuwezesha kumaliza masomo yake na kujikwamua kiuchumi na adhabu ya mtu atakayempa ujauzito mwanafunzi ama kukutwa naye nyumbani au katika nyumba ya kulala wageni ni kifungo cha miaka 30 jela.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi hususani waishio vijijini, wasikubali kurubuniwa na kugawa ardhi yao kwa watu mbalimbali wanaofika kwenye maeneo yao na kutaka wauziwe ardhi bila ya kuzihusisha mamlaka husika.
"Eneo lenu hili la Ilula ni zuri hivyo msikubali kurubuniwa kuuza ardhi yenu kwa sababau inathamani kubwa. Viongozi wa Kata na Vijiji hakikisheni mnaratibu vizuri na muandae mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro."
No comments:
Post a Comment