Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo wamewanyamazisha Kagera Sugar kwenye uwanja wao wa Kaitaba baada ya kuwafumua mabao 3-0 kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Kikosi cha kocha Patrick Aussems kilishuka dimbani leo kikiwa na nia moja tu, kudhihirisha umwamba wao dhidi ya Kagera Sugar ambao msimu uliopita walishinda michezo yote miwili dhidi ya Simba
Mapema tu kwenye dakika ya tano, Meddie Kagere aliitanguliza Simba kwa bao safi akiunganisha krosi ya Deo Kanda
Ilikuwa siku nzuri kwa Kagere ambaye ameendelea kuchanja mbuga kuelekea kiatu cha pili cha dhahabu
Kwenye dakika ya 35 Kagere alimtengenezea pasi murua Mohammed Hussein aliyeutumbukiza mpira kimiani kwa ustadi mkubwa
Simba ilikwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa mabao 2-0
Kipindi cha pili mabingwa hao wa Tanzania Bara waliendelea kutawala mchezo ambapo kwenye dakika ya 79 madhambi aliyofanyiwa Miraji Athumani ndani ya eneo la hatari yalipelekea mwamuzi kutoa adhabu ya mkwaju wa penati ambao uliwekwa kambani kwa shuti kali na Kagere
Ulikuwa ni mchezo ambao Simba ilionyesha ubora wa hali ya juu na kuwazima kabisa wapinzani wao ambao walikosa mbinu ya kuipenya ngome ya Simba iliyokuwa chini ya Paschal Wawa na Tairone Da Silva huku wakisaidiwa na kiungo mkabaji Gerson Fraga
Ushindi huo umeirejesha Simba kileleni mwa msimamo wa ligi
Simba inaelekea mkoani Mara ambako Septemba 29 itaikabili Biashara United

No comments:
Post a Comment