Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini Richard Kasesela, amelazimika kuomba radhi kwa umma, baada ya kusambaza taarifa za uongo juu ya kufariki kwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Dr. Salim Ahmed Salim.
Usiku wa kuamkia leo Septemba 30, 2019, Kasesela alichapisha taarifa kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter, ukieleza kutokea kwa kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Dr Salim zilizodai kuwa mauti hayo yamemfika akiwa nchini Uingereza, ambapo baadae alizikanusha.
"Kwa dhati naomba nimuombe radhi, Dr. Salim Ahmed Salim na kwa sasa bado yuko na anaendelea na matibabu nchini Uingereza nimeongea na familia, ni bahati mbaya sana chanzo kilichonipa habari hakikuwa sahihi, ninaomba radhi kwa familia na Watanzania kwa ujumla."ameandika Kasesela.
Mapema jana Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping alimtunuku Waziri Mkuu huyo mstaafu wa Tanzania Dkt Salim, kuwa miongoni mwa watu waliosaidia nchi hiyo kurejeshwa kwenye Jumuiya ya Umoja wa Mataifa.
EATV na EA Radio Digital, ilipomtafuta Mkuu huyo wa Wilaya,alijibu kwamba kwa sasa hawezi kulizungumzia kiundani kwa kuwa tayari ameshaomba radhi.
No comments:
Post a Comment