Mdee ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 4, 2019 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa baraza hilo uliowakutanisha wanawake wa chama hicho kujadili fursa na changamoto zilizo mbele yao kuelekea kwenye uchaguzi huo.
Mdee amesema katika uchaguzi wa mwaka 2015 wanawake sita pekee kati ya 64 waliojitokeza kugombea ubunge na kushinda.
Amebainisha kuwa wana uwezo wa kuongoza jamii, wanatakiwa kuungwa mkono na wanajamii wote ili nao wawe sehemu ya maamuzi kwenye ngazi za uongozi wa kata au mitaa wanapoishi.
"Kama tuna uwezo wa kuonyesha uongozi bora katika ngazi ya familia tukipanga na bajeti nini cha kutushinda,” amesema Mdee kwenye mkutano huo huku akishangiliwa na mamia ya wanawake.
Mdee amesisitiza kwamba huu ni wakati wa wanawake kuonyesha wao ni jeshi kubwa na wana nguvu kwenye chaguzi zinazofanyika kutokana na wingi wao.
" Msiposema na mkasikika na kuonyesha kwamba nyinyi ni jeshi kubwa hamtasikika. Mtaendelea kunyanyaswa na kubaki masikini. Takwimu zinaonyesha katika wanawake 100, 60 ni masikini wa kutupwa," amesema Mdee.
Kwa upande wake, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya amesema wanawake wanatakiwa kupendana na kuungana mkono katika harakati zote zinazofanywa na mwanamke mwenzao.
Bulaya amesema mshikamano, upendo na dhamira ya kweli ndiyo nguzo ya kuitoa CCM madarakani. Amewataka wanawake wa Chadema kupendana na kuona harakati za mwanamke mwenzao kama zao na chama chao.

No comments:
Post a Comment