Beki huyo si aliamua kukaa nyumbani akishinikiza kulipwa pesa za usajili kwani alikuwa hajapewa chochote tangu asaini mkataba mpya, huku pia akiwa na malimbikizo ya madeni kwa uongozi wa klabu hiyo na viongozi walishaanza kufikiria kumunguzia kiaina.
Hata hivyo, jana alikutana na mabosi wake kwenye makao makuu ya klabu hiyo ili kuwekana sawa, lakini mwishowe walishindwa kupata muafaka na jamaa kupanda zake bodaboda kurejea maskani akiwasikilizia viongozi hao.
Mwanaspoti lilipenyezewa kwamba mchezaji huyo aliitwa jana katika ofisi za klabu hiyo kwenda kuzungumzia suala la malipo yake ya usajili.
Baada ya kupata habari hizo lilienda kupiga kambi katika makao makuu ya Yanga na kumshuhudia Dante akiingia ndani majira ya saa sita mchana na kukaa kwa muda mrefu katika viti vya wageni kwa kuwa hakukuwa na kiongozi yeyote ofisini hapo.
Mwanaspoti likiwa limepiga kambi takribani saa mbili, ilipofika saa nane mchana, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Rogers Gumbo walifika klabuni hapo na kwenda kuzungumza na Dante - maongezi yaliyochukua takribani dakika 15.
Baada ya kutoka nje, Mwanaspoti lilimdaka mchezaji huyo na kumuuliza kikao hicho jinsi ambavyo kilikuwa, na walichokubaliana.Kwenye kikao hicho viongozi wa klabu hiyo walikuwa wanataka kujua namna ambavyo wataweza kumlipa pesa zake ili waweze kumalizana naye.
Dante alisema mazungumzo yao yalikuwa mazuri, lakini walijikuta wakishindwa kufikia muafaka baada ya kuambiwa akubali kupunguziwa pesa za usajili tofauti na walivyokubaliana wakati wanasaini mkataba kutokana na timu kutokuwa na pesa.
“Jamaa wamesema kwamba wao wanaweza kunilipa pesa nusu, kitu ambacho niliwaambia siwezi kukisema mpaka atakaporudi meneja wangu kati ya kesho au keshokutwa,” alisema. Kiongozi mmoja wa Yanga alikiri kuwa walizungumza na Dante, lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani wa mazungumzo yao.

No comments:
Post a Comment