Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally amesema hatashangaa kuona mbunge wa jimbo la Ilemela ambaye ni Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akipita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu ujao 2020 kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake.
Ameyasema hayo jijini Mwanza katika mkutano Mkuu wa Jimbo la Ilemela na kuelezea utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2015.
Amesema kuwa hakuna kumnadi tena Dkt. Angelina Mabula kwa kuwa anazo sifa zinazomuwezesha kutetea kiti chake na yeyote anayetaka kuwania nafasi katika jimbo hilo ajue kiti hicho kishakaliwa pamoja na kata zake 19.
‘’Ole wake anayetaka kupitia mlango wa nyuma, chama kina utulivu sitashangaa Dkt. Mabula akipita bila kupingwa uchaguzi ujao,‘’amesema Dkt. Bashiru.
Aidha, amewaonya wabunge wa CCM waliozembea kufanya ziara za kutatua kero za wananchi pamoja na kufanya vikao kwenye majimbo yao kuwa hawatakuwa na ulinzi wakati wa kinyanganyiro cha kupendekeza majina ya kuwania nafasi hizo na kusisitiza kuwa kipaumbele kitatolewa kwa wabunge waliokuwa wakichapa kazi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mabula amesema kuwa jimbo lake kwasasa limepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta za Elimu, Afya, Maji, Miundombinu, Uzalishaji na Mifugo, Viwanda na Biashara pamoja na Utamaduni na Michezo ukilinganisha na miaka iliyopita.
No comments:
Post a Comment