KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema wakuu wa mikoa na wilaya ambao wameshindwa kusimamia sheria ya mizani, wako hatarini kupoteza kazi zao.
Dk. Bashiru alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano mkuu maalumu wa CCM Wilaya ya Ilemela.
Mkutano huo uliandaliwa na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula ukiwa na lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM tangu mwaka 2015 hadi Machi mwaka huu.
Dk. Bashiru alisema Serikali haitaruhusu wakulima wake wanyonywe na wafanyabiashara kwa kutumia vipimo ambavyo havikubaliki kisheria, ikiwamo debe, mzani au gunia vilivyochezewa kwa lengo la kujipatia faida wakati inawalipa mishahara watumishi hao kusimamia na kulinda masilahi ya wananchi wake.
“Nashangaa tangu Serikali imetoa agizo hilo muda mrefu umepita, lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika, haki ya Mungu ninaapa, kuanzia leo RC na DC atakayeshindwa kusimamia unyonyaji huu hataendelea kuwa madarakani.
“Haiwezekani wao wapo, polisi wapo, lakini wakulima wetu wananyonywa kupitia vipimo vusivyo halali ikiwemo rumbesa halafu wanawapa bei ndogo zisizolingana na bidhaa waliyouziwa.
“Nimepita mikoa ya Mwanza na Shinyanga, nimeona jinsi wafanyabiashara wanavyoendelea kutumia rumbesa, kuanzia leo sitaki tena kuona unyonyaji huo unaendelea kwa wakulima wetu, hasa katika mazao ya dengu na kahawa,” alisema.
Aliwaagiza pia wakuu wa mikoa na wilaya ambazo zinalima pamba kusimamia zao hilo kikamilifu ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu namna bora ya kuitunza ili ikidhi vigezo vya ubora katika soko la dunia.
Kwa upande wake Mbunge wa Ilemela, Mabula, alisema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM mwaka 2015/2020 katika jimbo hilo na ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati akiomba kura mwaka 2015 umefanikiwa kwa asilimia 95, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, afya na elimu.
No comments:
Post a Comment