Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa Seleman Jafo amesema wasichana wote waliofaulu katika mtihani wa kidato cha Nne katika mwaka uliopita wa 2018 wamefanikiwa kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo mbali mbali vya ufundi nchini.
Jafo, ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akitangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi kwa mwaka wa masomo utakaoanza mapema mwezi Julai, 2019.
Akitoa takwimu za ufaulu wa watahiniwa wa kidato cha Nne kwa mwaka 2018, kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu, alisema ni watahiniwa 113,825 kati yao wasichana ni 47, 779 na wavulana 66,046 sawa na asilimia 31.76 ya watahiniwa wote waliofanya mtihani.
“Nipende kuwatangazia habari njema kuwa, kwa mwaka huu wasichana wote waliofaulu wamefanikiwa kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano pamoja na vyuo mbali mbali vya ufundi, ambapo jumla yao ni wasichana 45,816", amesema Waziri Jafo.
Waziri Jafo, amewataka Wanafunzi wote waliochaguliwa kuzingatia maelekezo yote muhimu ikiwepo kuthibitisha kabla ya tarehe ya mwisho hususani kwa wale watakao jiunga na vyuo vinavyo simamiwa na (NACTE).
“Tumetoa tarehe kuanzia Julai 8 2019 hadi 30 Agosti, wote wawe wamethibithisha kujiunga katika vyuo vya ufundi na watakaoshindwa kufanya hivyo nafasi zao zitajazwa na wanafunzi wengine", ameongeza Waziri Jafo.
No comments:
Post a Comment