Uongozi wa Simba umewaleta nchini mshambuliaji wa TP Mazembe, Deo Kanda aliyetua jana Ijumaa pamoja na Mtogo Serge Alainnogue
Wawili hao wako kwenye mazungumzo na huenda wakasajiliwa kutegemeana na mipango ya mabingwa hao wa Tanzania Bara
Kulingana na Mwanaspoti, Deo Kanda anatajwa kuja kuchukua nafasi ya Okwi ambaye kuna uwezekano mdogo wa kuendelea kubaki Msimbazi
Kanda mwenye umri wa miaka 29 ubora wake umeifanya TP Mazembe kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa, kwani ni mkali wa kufumani nyavu tangu alipoanza kuichezea 2009 na 2013 alitimka kwenda Raja Casablanca ya Morocco aliyocheza kwa msimu mmoja.
Alirudi DR Congo na kuichezea AS Vita msimu mmoja wa 2014-2015, akatimkia tena Ugiriki alipojiunga na AEL, lakini hakudumu kwani msimu huo huo alirejea Mazembe akiichezea mpaka sasa na Simba ilimuona walipovaana na Mazembe katika mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Kwa upande wa Mtogo Serge mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za winga pamoja na namba 10, alitumiwa tiketi na Simba wiki iliyopita na kufichwa jijini Dar akiendelea na majadiliano.
Dogo huyo mwenye miaka 18, anatoka Klabu ya Glory, alitua na Ndege ya Shirika la Ethiopia, ingawa taarifa zilizonaswa jana ni kwamba anaendelea kujifua akiwa na KMC kwa vile Simba kwa sasa haijaanza maandalizi na hataki kushusha kiwango chake.
Inaelezwa Simba inataka kumsajili mchezaji huyo ambaye kulingana na umri wake malengo yao ni kumwendeleza kama ilivyowahi kufanya kwa Okwi alipotua kwa mara ya kwanza au kama ilivyokuwa kwa Mnigeria Eme Ezechukwu aliyesajiliwa mwaka 2008.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alifichua kuwa, usajili wao unafanywa kwa mapendekezo ya kocha wao, Patrick Aussems na kama mahitaji yao yatatosha zoezi kwa wageni litaishia walipofikia sasa, lakini kama matahitaji kwa wachezaji hao hayatatosha wanaweza kuwasajili wengine.
No comments:
Post a Comment