Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole amefanya ziara ya kukagua na kufuatilia mradi wa kufua umeme katika kituo cha kufua umeme wa gesi cha Somanga Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ambapo amesema Chama kimeridhishwa na maendeleo ya ufuaji wa umeme katika kituo hicho.
Akifafanua zaidi Polepole amesema Chama kiliahidi kurudi Kilwa baada ya wananchi kukipatia ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu na Uchaguzi mdogo wa marudio na kuwa kinaendelea kufuatia pamoja na ahadi zingine upatikanaji umeme katika maeneo ya Miteja, Nangurukuru,Kilwa, Somanga na Lindi mjini ambayo yanahudumiwa na kituo cha kufua umeme Somanga.
“Tungependa Viongozi na watendaji wa Serikali wakiwemo Mawaziri waendeleze utamaduni mzuri wa kusimamia na kutekeleza ahadi za Chama katika maeneo yote kwani huo ndio msingi wa wananchi kuendelea kutupenda na kutupatia dhamana ya uongozi” amesisitiza Ndg. Polepole.
Huu ni muendelezo wa ziara za kukagua na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020.
No comments:
Post a Comment