Watu 26 wamethibitishwa kufa ndani ya siku moja kwenye jimbo la Kivu Kaskazini Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na maradhi ya Ebola yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo.
Mlipuko wa sasa wa Ebola ni wa pili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa baada ya ule uliokumba maeneo ya Afrika Magharibi mwaka 2014-2016 na kuua watu zaidi ya elfu 11.
Wizara ya Afya ya DRC imethibitisha vifo vya watu 957 huku ikirekodi visa vya watu 891 ambao wameambukizwa maradhi ya Ebola nchini humo. Serikali ya Kinshasa imetangaza mikakati zaidi ya kukabiliana na kuenea kwa maambukizi zaidi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeendelea kukabiliwa na vizingiti kutokana na makundi ya waasi kushambulia vituo vya afya vinavyotoa matibabu kwa wagonjwa wa maradhi hayo.
Hivi karibuni kundi la wanamgambo lilishambulia kituo kimoja cha afya huko Butembo ikiwa ni masaa machache tu baada ya shambulio jingine kama hilo lililopelekea daktari mmoja kutoka Cameroon kuuawa. Kufuatia hali hiyo ya kukosekana usalama, madaktari wanaofanya juhudi za kuwatibu raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaougua maradhi ya Ebola wametishia kufanya mgomo endapo watashambuliwa tena.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa, hakuna dalili za ugonjwa wa Ebola kupungua katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bali kinachotazamiwa ni kuwa, ugonjwa huo utazidi kuenea nchini humo.
No comments:
Post a Comment