Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa wamempa siku saba mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi kuwaomba radhi baada ya kuwataka nao kuwa na vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo
Akizungumza hapo jana Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Iringa, Frank Leornald amesema kauli ya Hapi inadhalilisha taaluma ya habari
Leornald amesema waandishi wa habari mkoani humo wamefanya majadiliano na kuazimia mambo sita watakayoyawasilisha katika ofisi ya mkuu huyo wa Mkoa, na kutaka majibu ya haraka
“Tumesikitishwa kuwekwa katika kundi moja linalolinganisha taaluma ya habari na wafanyabiashara. Katika maazimio hayo sita tumemuomba Hapi kutoa tafsiri rasmi anayoijua yeye kuhusu waandishi rasmi na wasio rasmi.”
“Tunaamini taaluma ya habari ni kama taaluma nyingine za sheria, udaktari na ualimu hivyo kuingiza wanahabari katika kundi la wafanyabiashara wanaotakiwa kuwa na hivyo vitambulisho ni kuidhalilisha taaluma yetu,” amesema Leornald.
Utakumbuka Mei 27, 2019 wakati akizungumza na watendaji wa Serikali kuhusu ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara, RC Hapi aliwataja waandishi wa habari kama wafanyabiashara na vibarua wasio rasmi, huku akianisha makundi 53 yanayostahili kupata vitambulisho hivyo.

No comments:
Post a Comment