Kocha Mkuu wa Azam FC Meja Jenerali Mstaafu Abdul Mingange amesema usimamizi mbovu wa TFF kwa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu, umepelekea ligi hiyo kukosa ushindani na kupatikana kwa bingwa wa 'mashaka-mashaka'
Akizungumza jana baada ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya Azam Fc uliomalizika kwa timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, Mingange amesema ligi ya msimu huu ndio ligi mbovu aliyowahi kuishuhudia katika maisha yake ya ukufunzi wa mpira wa miguu
"Sio ligi iliyofurahisha kabisa, ni ligi mbovu kuiona katika maisha yangu tangu nilipoanza kusimamia mpira," alisema Mingange
"Ni ligi ambayo haina udhamini, ligi ambayo haina sheria, ligi ambayo haifuati taratibu, ligi ambayo mwingine ana mechi 20 mwingine ana mechi tano, sijawahi kuona duniani ligi ya namna hii"
"Kwa hiyo lazima tuseme kwamba si ligi nzuri na chama cha mpira kiangalie"
"Kwa mwenendo huu si rahisi kumpata bingwa ambaye ni halali kwa sababu kama mtu ameshacheza mechi, zilizobaki anacheza tu amalizie na timu nyingi ni maskini zinaweza kujichezea tu"
"Nyingine zinapeleka timu uwanjani bila ya kufanya mazoezi kwa hiyo upinzani ulikosekana kwa yule ambaye alikuwa na mechi nyingi, na hicho ndicho nilichokiona"
Alichokizungumza Meja Jenerali Mstaafu Mingange kimedhirika katika baadhi ya michezo mfano mchezo kati ya Simba dhidi ya Coastal Union uliopigwa uwanja wa Uhuru na Coastal Union kubugizwa mabao 8-1
Coastal Union iliwasili jijini Dar es salaam kutoka Tanga masaa mawili kabla ya mchezo hilo likidhihirisha kuwa timu hiyo haikuwa na lengo la kushindana bali kukamilisha ratiba tu
Mara kwa mara kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alitoa malalamiko ya aina hiyo juu ya uendeshaji wa ligi lakini alijikuta akiitwa kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF
Ni dhahiri TFF na Bodi yake ya Ligi wanapaswa kujisahihisha na kuhakikisha msimu ujao wanasimamia kanuni na sheria ili kuweka ushindani ulio sawa kwa timu zote

No comments:
Post a Comment