Mbunge wa Kahama Mjini kupitia CCM, Jumanne Kishimba, ameshangazwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliojitokeza wakiwania nafasi 70 kwenye Mamlaka ya Mapato ya Tanzania TRA ambazo zilitangazwa hivi karibuni.
Akichangia kwenye mjadala wa Wizara ya Elimu, Mbunge Kushimba, amehoji juu ya kundi hilo kubwa la wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 40000 kukosa uwezo wa kujiajiri, huku wakiwa wamehitimu elimu ya juu.
"Juzi TRA ilitangaza nafasi 70, lakini waliojitokeza ni wanafunzi 40000, suala hili Wizara ya Elimu ilitakiwa iogope na isikitike sana, kwa sababu wangejiuliza hawa wanafunzi wengine wataenda wapi baada ya hawa 70 wakishapata kazi", amesema Kishimba.
"Kwetu sisi wanaomaliza shule wanaweza kuwa milioni 1, lakini wanaopata ajira ni wanafunzi 50000 tu, na Mkapa alishaliongea hili suala lakini halijapewa kipaumbele sana, ni vizuri watunga sera wakatunga sera mpya, ili wanafunzi wafundishwe shughuli za nyumbani kuwa ni hela", ameongeza Mbunge Kishimba.
Aidha Mbunge Kishimba ameendelea kusema,"wewe umechukua hela zake, milioni 10 za "University" halafu ukampa shahada, wewe unavyosema lakini ni sawa na umempa karatasi tu, mimi mwenyewe ni muathirika mkubwa wa digrii, na nina watoto 6 wana "degree" bora, vyuo vikuu vingeanza kutafuta ajira kwanza, ndiyo vitangaze nafasi za masomo, kule mtaani mambo ni magumu".
No comments:
Post a Comment