VYOMBO vya habari vya Korea Kusini hii leo vimeripoti kwamba Korea Kaskazini imemuua mjumbe wake maalumu kwa ajili ya Marekani Kim Hyok Chol kufuatia kushindwa kwa mkutano wa pili wa kilele kati ya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais Donald Trump.
Gazeti la Chosun Ilbo limeandika Chol aliyeuandaa mkutano huo wa Hanoi na kumsindikiza Kim kwenye treni yake binafsi ameuawa kwa kupigwa risasi kwa kile kinachotajwa kumsaliti kiongozi huyo wa juu baada ya kufanikiwa kuishawishi Marekani wakati wa majadiliano ya kabla ya mkutano huo wa kilele.
Gazeti hilo lililonukuu chanzo ambacho hakikutambulishwa limesema Chol, aliuawa mwezi Machi, katika uwanja wa ndege wa Mirim pamoja na maafisa wanne waandamizi wa wizara ya mambo ya nje baada ya uchunguzi.
Mkalimani wa Kim kwenye Umoja wa Mataifa naye ametiwa kizuizini baada ya kufanya makosa kwenye mkutano huo wa kilele.
No comments:
Post a Comment