YANGA imemshusha nchini kimyakimya straika wa FC Lupopo, Rodrick Mutuma na watamalizana nae kwa siri sana arejee DR Congo. Mchezaji huyo raia wa Zimbabwe, ni miongoni mwa wachezaji walioko kwenye rada ya Mwinyi Zahera ambaye amepanga kukamilisha usajili wa Yanga mwezi ujao.
Tayari kocha huyo mwenye uraia wa Ufaransa ameshapewa advansi aliyotaka ya Sh.Mil 80 kumalizana na baadhi ya wachezaji wakae mkao wa kula.
Habari za uhakika ambazo Spoti Xtra imezipata ni kwamba Mutuma aliyeifungia timu yake bao pekee katika mechi ya ligi dhidi ya TP Mazembe msimu huu, ametua Dar es Salaam wiki iliyopita kwa maagizo ya Zahera na kwamba atamaliza dili yake wikiendi hii kwa siri.
Mmoja wa viongozi wa Yanga aliidokeza Spoti Xtra kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na hali halisi iliyoko klabuni na wanataka kumalizana na wachezaji wote muhimu kwa wakati. Habari zinasema kwamba mchezaji huyo amefichwa na moja ya hoteli Jijini Dar es Salaam na haipaswi kuvuja mpaka msimu umalizike.
Alisema kwamba wanahofia ishu ikivuja itawavunja moyo baadhi ya wachezaji ambao hawana uhakika wa kusalia Jangwani msimu ujao kutokana na sababu mbalimbali. Habari zinasema kwamba baadhi ya wachezaji ambao wako kwenye mazungumzo ya mwisho na Yanga wameanza kuwauliza marafiki zao ndani ya klabu hiyo hali ilivyo, jambo ambalo limewatia hofu viongozi kwamba inaweza kuleta tena mgomo kama wa juzi.
Yanga tayari imefikia makubaliano ya awali na kipa wa Bandari ya Kenya, Farouk Shikalo lakini inaendelea kuwashawishi Yanick Litombo wa AS Vita na Jacques Tusiyenge wa Gormahia ambaye wakala wake ameshawatajia dau la mteja wake.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba Zahera amewaambia viongozi kwamba dili zote atamaliza mwenyewe kimyakimya wakati akiendelea kupambana kupata Kombe la FA ili wapate upenyo wa kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
Zahera anataka kukamilisha usajili wake kwa asilimia kubwa kabla ya kuanza kwa michuano ya Afcon, Juni 21 nchini Misri ambapo atakuwa bize na DR Congo. Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba kwa mara ya kwanza msimu huu wachezaji wote wanaotoka Yanga watajua hatma zao kabla ya kumalizika kwa msimu.
Chanzo: GPL
No comments:
Post a Comment