Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefunga mitambo yote ya kuchenjulia madini ya dhahabu Wilayani Kahama baada ya kubaini udanganyifu mkubwa kwenye uchenjuaji wa madini.
Naibu Waziri Nyongo amechukua hatua hiyo kwenye ziara yake aliyoifanya jana Wilayani Kahama yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Akiwa katika ziara hiyo, alifanya ziara ya kushtukiza katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group inayomilikiwa na Theogenes Zacharia pamoja na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Antidius na kubaini kampuni hiyo imekuwa ikiwaibia wateja wake kupitia mfumo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu.
Naibu Waziri alioneshwa na wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini waliopewa kazi maalum ya kuchunguza mfumo wa uchenjuaji wa dhahabu wa kampuni hiyo, sehemu ya mabomba ya mfumo iliyoharibiwa kwa makusudi kwa lengo la kunasa kiasi cha dhahabu kabla ya kufikishwa katika chombo maalum cha kupokelea kwa ajili ya mteja.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Kamishna Msaidizi, Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Saidi Ali, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Andrea Fabian, wataalam kutoka Tume ya Madini, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment