Mbunge Jimbo la Ndanda Cecil Mwambe (CHADEMA) amemkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli mkoani Mtwara ambapo anatarajiwa kuwa na ziara ya siku mbili.

Cecil Mwambe
Katika Ukaribisho wake, Mbunge Mwambe amemsihi Rais Magufuli kuonana nae kabla hajafika ili aweze kuzungumza nae kuhusu suala la malipo ya korosho.
"Mh. Raisi Magufuli karibu sana Mtwara, niongee na wewe kabla haujafika, watu wa uko wanatamni kusikia ni lini serikali itawalipa pesa yao, ahadi ya mwisho ilikuwa tar 31, karibu sana", amesema Mwambe.
Wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema Aprili 2, Rais Magufuli anatarajia kufungua na kuweka mawe ya msingi ikiwemo kwenye Uwanja wa Ndege wa Mtwara, ujenzi wa barabara ya Mtwara hadi Mnivata na kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin mkoani humo.
Aidha, alisema Aprili 3 mwaka huu, kiongozi huyo wa nchi ataweka jiwe la msingi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha Ualimu Kitangali wilayani Newala. Pia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mbonde wilayani Masasi pamoja na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wilayani humo.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Aprili 4, mwaka huu, atafanya uzinduzi wa mradi wa barabara ya Mangaka hadi Nakapanya kuelekea Tunduru na Mangaka hadi Mtambaswala.
No comments:
Post a Comment