Inaelezwa uongozi wa Yanga bado haujakata tamaa kumnasa mlinda lango wa Bandari Fc Farouk Shikalo ambaye pia yuko katika kikosi cha timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars
Shikalo alikaribia kutua Yanga wakati wa usajili wa dirisha dogo kabla ya dili lake kukwama kwenye dakika za majeruhi kutokana na ukosefu wa fedha
Kushindikana kwa usajili wa Shikalo na wachezaji wengine watatu wakati wa dirisha dogo, kulimkera Zahera aliyewatupia lawana Kamati ya usajili ya Yanga kwa kumdanganya kuwa walikuwa wamefanikisha usajili wa wachezaji hao
Hata hivyo ili kuhakikisha Yanga haishindwi kusajili kutokana na ukosefu wa fedha, Zahera alibuni mkakati wa kukusanya fedha kwa ajili ya usajili, zoezi ambalo linaendelea sasa kwa kuwashirikisha wadau wote wa klabu ya Yanga
Yanga imepanga kutumia Bil 2 kwa ajili ya kuboresha kikosi chake mwishoni mwa msimu, fedha ambazo zinakusanywa kutoka kwa wadau kupitia michango yao
Sasa habari njema ni kuwa Shikalo amegoma kuongeza mkataba katika klabu yake ya Bandari Fc ikiwa ni makubaliano na Yanga inayokusudia kumsajili mwezi Mei
Mmoja wa viongozi wa Yanga amenukuliwa na Mwanaspotiakisema kuwa walikubaliana na mlinda lango huyo kuwa asiongeze mkataba wake na Bandari Fc kwani wamedhamiria kumsajili mwishoni mwa msimu
"Bado tuna akili ya kuchukua kipa na bado tunafanya mawasiliano na Farouk unajua usajili wake wakati ule ulikwama kutokana na upungufu wa fedha klabu yake ilihitaji fedha nyingi.
"Tumemwambia kwamba asiongeze mkataba asubiri hadi Mei mwaka huu tuangalie kipi tutakubaliana na klabu yake, unajua akiongeza bei yake itakuwa juu zaidi na kama akifanya hivyo inamaana tutaachana naye na tuangalie kipa mwingine."
Mkataba wa Shikalo na Bandari Fc unamalizika mwezi Disemba mwaka huu.
Itakapofika mwezi Juni mkataba huo utakuwa chini ya miezi sita na hivyo ataruhusiwa kufanya mazungumzo na timu yoyote.
Kama Bandari Fc itahitaji dau kubwa, Yanga inaweza ikasubiri mkataba wake umalizike kabisa mwezi Disemba ili imsajili akiwa mchezaji huru
Shikalo ni chaguo la kwanza la kocha Mwinyi Zahera anayetafuta mbadala wa Beno Kakolanya ambaye atatua klabu ya Simba mwishoni mwa msimu baada ya kuvunja mkataba wake na Yanga
No comments:
Post a Comment