Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewaomba radhi Watanzania wote waliojitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa juzi kushuhudia mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika, Afcon 2019 na kushindwa kuingia kutokana na uwanja kujaa.
Stars, juzi iliifunga Uganda mabao 3-0 na kufuzu fainali za Afcon zilizopangwa kufanyika Misri Juni mwaka huu.
Tanzania imefuzu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39. Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, mashabiki walikuwa wengi na kujaa uwanjani mpaka ikatangazwa milango ifungwe wasiingie tena hivyo wengi walibaki nje na wakati mwingine polisi walilazimika kuwatawanya na mabomu ya machozi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Lindi, Mwakyembe amesema wizara yake inaichukua changamoto hiyo kama funzo na katika mechi za Kimataifa zijazo itahakikisha inaweka runinga kubwa na nyingi kwenye viwanja vingine ili watakaokosa nafasi ya kuingia nao waone mechi husika.
"Mimi kwa sababu naiongoza wizara ya habari na michezo, niwaombe radhi watanzania waliomiminika uwanja wa taifa wakakosa nafasi," alisema Waziri Mwakyembe.

No comments:
Post a Comment