Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Dk. Bashiru Ali amesema kuwa anatamani kushuhudia hatima ya ndoa ya kisiasa ya Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif na kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kutokana na viongozi hao kuungana ilihali wana amini katika Sera za mlengo tofauti.
Amesema kuwa wanasiasa hao wanasifika kwa kuwa na misimamo tofauti ambapo Maalim ni muumini wa muungano wa mkataba huku Zitto akijinadi kufuata msimamo wa ujamaa wa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa akiamini katika muungano.
Dk.Bashiru ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua Mkakati wa Kuimarisha Demokrasia Mashina na matawi, amesema kuwa misimamo ya wanasiasa hao ipo tofauti kabisa.
Amesema kuwa Maalim, msimamo wake kuwa muungano ni unyonyaji, ukoloni na anadai njia pekee ni muungano wa mkataba.
Aidha amesema kuwa CCM hakitishwi na kile kinachoitwa mafuriko ya kisiasa kwani inauzoefu wa kuhimiri kwa kuwa ina mifumo thabiti ya uongozi.
Dk.Bashiru amesema kuwa anashangaa kuona chama kina mbunge mmoja Tanzania bara lakini kinajinadi mwakani kitaongoza nchi kutokana na kuwa na waafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii.
“CCM hakifanyi mikakati yake kwa kupitia Mitandao ya kijamii kwani haipigi kura, hivyo CCM haiwezi kuogopa mitandao ya kijamii. sisi tunakwenda kimkakati na sio kimafuriko”amesema Dk.Bashiru
Hata hivyo amesema kuwa mwaka jana CCM ilikuwa ina test mitambo ila Mwaka huu mitambo ipo tayari na inaanza mashambulizi kwani ugonjwa wa fitina na marumbano Rais Dk. Magufuli ameuponyesha na sasa umehamia upinzani.
Aidha Dk.Bashiru ameuagiza Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwenda mkoani Kigoma kisha wamalizie Kilimanjaro huku Arusha tayari Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ameshamaliza kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoani Dodoma,Godwin Mkanwa,ameeleza kuwa mkakati huo ni kutaka kuwafahamisha wana CCM kuwa Dodoma inaunga mkono kwa vitendo juhudi za rais katika kuimarisha chama na serikali.
Mkanwa amesema kuwa viongozi hao wa mashina watapewa mafunzo ili waweze kufahamu majukumu yao kwa lengo la kuzuia mgongano wa kimajukumu.
Naye Katibu wa CCM mkoa huo, Jamila Yusuph, ameeleza kuwa Dodoma itaendelea kuwa ngome imara ya Chama Cha Mapinduzi.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoani Dodoma, Mzee Job Lusinde, alikumbusha umuhimu wa kutunza nembo za chama na serikali.
“Kuna sehemu nilienda nikakuta bendera inayopepea si ya Tanzania kutokana na uchakavu wake kwani ilikwisha poteza maana. Alama hizi hazipaswi kuwa biashara kwa kutengeneza bendera kwa kutumia vitambaa ambavyo havina ubora,” amesema Mzee Lusinde.


No comments:
Post a Comment