Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi yake ya haraka ya kupeleka misaada ya kibinadamu kwa nchi za Zimbabwe, Malawi na Msumbiji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mussa Zungu ameyasema hayo mjini Dodoma wakati kamati yake ikipokea taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Mheshimiwa Waziri, tufikishie pongezi zetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa busara, hatua na maamuzi yake ya haraka ya kupeleka misaada ya kibinadamu kwa majirani zetu waliopatwa na maafa, mikono inayotoa ni bora zaidi kuliko midomo inayozungumza, Mheshimiwa Rais ameonesha uungwana na ubinadamu mkubwa sana” alisema Mhe. Zungu.
Akipokea pongezi hizo za bunge kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi (Mb.), amesema ni jambo la kutia moyo kuona Kamati ya Bunge inatambua jitihada za Mheshimiwa Rais za kudumisha ujirani mwema, undugu na mshikamano kwa jirani zetu.
“Salam tulizozipata tutazifikisha kwa Mheshimiwa Rais kwa unyenyekevu mkubwa sana, ni jambo la kutia moyo kuona kuwa Kamati inatambua jitihada alizozifanya Mheshimiwa Rais na taarifa tulizozipata ni kuwa hali ya Msumbiji bado si nzuri sana” alisema Profesa Kabudi.
Aidha, Profesa Palamagamba Kabudi amewahamasisha wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu kuwa waaminifu na kupeleka sokoni dhahabu nzuri bila ya ujanja ujanja ili kuitumia vizuri fursa ambapo nchi ya Qatar imeonesha nia ya kununua dhahabu ya wachimbaji wadogo wadogo katika soko lililoanzishwa hivi karibuni. Nchi ya Qatar imeonesha nia hiyo, kutokana na mazungumzo kati ya Mheshimiwa Rais na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar wakati wa ziara yake nchini hivi karibuni.
“Tuwe waaminifu, tulete dhahabu nzuri na tushiriki kikamilifu ili hawa ndugu zetu wa Qatar wakishakuwa na imani na sisi watainunua dhahabu hii na wachimbaji wadogo wadogo watakuwa na uhakika na soko la dhahabu tofauti na ilivyo sasa”
Serikali ya Tanzania ilipeleka misaada kwa nchi hizo kufuatia kukumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga kijulikanacho kama Idai. Misaada hiyo ni pamoja na madawa ya binadamu na chakula.

No comments:
Post a Comment