Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali pingamizi la Serikali kupinga Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko kusikilizwa shauri lao la kuomba kupewa dhamana katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam
Hukumu hiyo iliyoandaliwa na jopo la majaji watatu Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika na Mwanaisha Kwariko, Februari 18 mwaka huu, imesomwa leo Ijumaa, Machi Mosi, 2019 na Naibu Msajili Sylvester Kainda.
Akisoma hukumu hiyo Naibu Msajili Kainda amesema hoja za rufaa za DPP kwamba Jaji wa Mahakama Kuu alikosea kuamua kusikiliza rufaa ya kina Mbowe bila kuambatanisha na mwenendo wa uamuzi wanaoupinga na kwamba alinyimwa fursa ya kusikilizwa kwa usawa hazina mashiko.
Baada ya kutupilia mbali rufaa hiyo ya DPP, Mahakama ya Rufani imeelekeza jalada la rufaa hilo lirejeshwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya kina Mbowe kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana.
Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.
Wawili hao walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kwa Jaji Sam Rumanyika.
Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.
Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu.
No comments:
Post a Comment