Tunatoa wito kuwahamasisha wananchi wote wenye sifa za kuwa wapiga kura katika kata za Kibutu (Kisarawe, Pwani) na Kihonda (Morogoro mjini) kujitokeza kwa wingi kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) kuanzia kesho Ijumaa, Machi 29, 2019, yakiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Chadema inahamasisha wananchi kujitokeza na kujiandikisha kwa wingi, ikitambua pia kuwa NEC imekiuka Katiba ya Nchi na Sheria ya Uchaguzi zinazoipatia mamlaka ya kuratibu na kusimamia uandikishaji wa wapiga kura nchini.
Wakati ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaipatia NEC mamlaka hayo kwa Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Madiwani kwa Tanzania Bara, Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343, kifungu cha 15(5) na kifungu cha 21(5) kinaiamuru NEC kuboresha DKWK mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na unaofuata. Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, NEC haijatekeleza takwa hilo la kisheria na hakujawahi kutolewa taarifa yoyote rasmi kwanini daftari halijaboreshwa kama sheria inavyoagiza.
Kupitia taarifa hii, tunaitaka NEC iwaeleze wadau wa uchaguzi na Watanzania wote kwanini hadi sasa haijaboresha DKWK na pia itoe ratiba ya shughuli ya uandikishaji wapiga kura kwa nchi nzima.
Uandikishaji wa majaribio unaoanza kesho katika kata hizo mbili, unafuatia tangazo lililotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia kwa Mwenyekiti Jaji Semistocles Kaijage, unatarajiwa kufanyika kwa siku 8, kuanzia Machi 29 - Aprili 4, mwaka huu katika maeneo hayo yaliyotajwa.
Shughuli hiyo itakayofanyika kwenye vituo 20 ambavyo vimegawanywa katika vituo 10 kwa kata hizo mbili, inalenga kufanyia majaribio vifaa na mfumo wa uandikishaji daftari hilo ili kubaini changamoto zake, kabla ya kuanza rasmi katika maeneo yote nchi nzima.
Tunawasihi na kuwahamasisha wakazi wa maeneo ya Kibutu na Kihonda, waliofikisha miaka 18 au wanaotarajia kufikisha umri huo mwaka kesho wakati wa kupiga kura, ambao ni raia wa Tanzania, wajitokeze kwa wingi, wakionesha mfano kwa Watanzania wengine umuhimu wa shughuli hiyo. Halikadhalika tunatoa wito pia kwa wapiga kura wote katika maeneo hayo waliokuwa wameandikishwa kupiga kura uchaguzi mkuu wa 2015, nao wafike katika vituo hivyo kuhakiki taarifa zao. Aidha wote waliopoteza vitambulisho vyao na wale ambao vitambulisho vyao vimeharibika au wamehamia makazi katika maeneo hayo kufika katika vituo hivyo kwa ajili ya utaratibu wa kuandikishwa.
Chadema tayari imeshaweka utaratibu wa kuwa na mawakala katika vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura kama taratibu zinavyoelekeza.
Kwa kutambua umuhimu na unyeti wa uandikishaji wa wapiga kura kama hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi, hasa Taifa linapojiandaa na uchaguzi mkuu wa 2020, Chadema kimejipanga kushiriki na kufuatilia shughuli hiyo kwa ukaribu na umakini unaohitajika.
Imetolewa leo Alhamis, Machi 28, 2019 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema.

No comments:
Post a Comment